Alikiba afichua kazi yake ya kando ambayo imemuingizia kipato kikubwa

Alikiba alisema ingawa haijakuwa safari rahisi, kwa bahati nzuri ameweza kuvuna matunda ya jasho lake.

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo alifichua kwamba kwa muda mrefu amekuwa akifanya kilimo cha biashara kwa faragha.

•Alikiba aliwashauri vijana kujitosa kwenye ukulima wa biashara huku akiwahakikishia kuna pesa nyingi pale

Mwimbaji Alikiba kweny shamba lake la nyanya
Image: INSTAGRAM// ALIKIBA

Staa wa Bongo Ali Saleh Kiba almaarufu Alikiba amefichua moja ya kazi zake kuu za kando.

Katika taarifa yake ya siku ya Jumapili, mwanamuziki huyo alifichua kwamba kwa muda mrefu amekuwa akifanya kilimo cha biashara kwa faragha.

Bosi huyo wa Kings Music alibainisha kuwa ingawa haijakuwa safari rahisi, kwa bahati nzuri ameweza kuvuna matunda ya jasho lake.

"Kwa muda mrefu nimewekeza kwenye kilimo na kiukweli imekuwa experience ya tofauti iliyojaa changamoto lakini yenye mkwanja kinoma," alisema.

Aliongeza, "Nimesukumwa sana ku-share hii na vijana wenzangu ili kuunga Mkono jitihada za Bi. Mkubwa kwa Vijana wenzangu sababu nakiona Kilimo kuwa ni kitu cha uhakika kinachoweza kubadili life yetu."

Mwimbaji huyo mkongwe aliambatanisha taarifa yake na picha kadhaa zilizomuonyesha akiwa kwenye shamba la nyanya. Alionekana akizunguka kukagua shamba hilo na hata kuchuma baadhi ya mazao.

Kufuatia hilo, mwimbaji huyo mkongwe aliwashauri vijana kujitosa kwenye ukulima wa biashara huku akiwahakikishia kuna pesa nyingi pale. Pia aliahidi kuwapeleka mashabiki wake katika safari yake ya kilimo kama njia ya kuwatia moyo.

Alisema kufunguka kuhusu biashara yake nyingine ni hatua kubwa kwani amekuwa akipendelea kuweka maisha yake nje ya muziki kuwa siri.

"Wengi wanaonifahamu wamenifahamu kupitia muziki wangu. Hii haijatokea kwa bahati mbaya coz maisha yangu nje ya muziki kwa kiasi kikubwa niliamua kuyaacha yawe ya kibinafsi," alisema.

Alikiba ni miongoni mwa wasanii tajika, sio nchini Tanzania pekee yake, bali pia kote Afrika Mashariki na nje ya mipaka yake. Amekuwa kwenye tasnia ya muziki kwa takriban miongo miwili na ameendelea kuonyesha ubabe wake uandishi na uimbaji.