Esther Musila afichua maombi maalum aliyofanya kabla ya kukutana na Guardian Angel

Musila alidokeza kuwa Mungu alijibu maombi yake kwa kumletea Guardian Angel.

Muhtasari

•"Niliomba kwamba wakati nitafikisha miaka 50 mwaka wa 2020, Mungu abadilishe maisha yangu kabisa," Bi Musila alisema.

•Esther Musila alisema wimbo wa mwimbaji huyo wa injili, 'Rada' ulikuwa mwanzo wa muungano wao wa kudumu.

Image: INSTAGRAM// ESTHER MUSILA

Bi Esther Musila amedokeza kwamba aliombea muungano wake na mwimbaji wa nyimbo za injili Peter Omwaka almaarufu Guardian Angel.

Akizungumza kwenye video ambayo alipakia siku ya Jumatatu, mama huyo wa watoto watatu wakubwa alifichua kuwa takriban miaka minne iliyopita, aliomba dua kwa Mungu na kumsihi abadilishe maisha yake.

"Niliomba kwamba wakati nitafikisha miaka 50 mwaka wa 2020, Mungu abadilishe maisha yangu kabisa," Bi Musila alisema.

Musila alisema aliendelea kusali na kumwomba Mungu afanye mapenzi yake kwake na kumpa maana maishani. Alidokeza kuwa Mungu alijibu maombi miezi michache baadaye kwa kumletea mumewe Guardian Angel maishani.

“Mume wangu Peter Omwaka, namshukuru Mungu kwa ajili yako, namshukuru Mungu kwa kukuleta katika maisha yangu, kwa kukutumia kubadilisha maisha yangu, kwa kunionyesha upendo na unyenyekevu na kuyafanya maisha yangu kuwa mazuri,” alisema.

Mhasibu huyo mwenye umri wa miaka 53 alisema hayo huku akiadhimisha miaka mitatu tangu alipokutana na Guardian Angel siku ya Jumatatu, Machi 13, 2023.  Alisema tarehe 13 mwezi Machi daima itasalia kuwa maalum na ya maana kwake.

Esther Musila alisema wimbo wa mwimbaji huyo wa injili, 'Rada' ulikuwa mwanzo wa muungano wao wa kudumu. Alipata hamu ya kukutana na Guardian Angel baada ya kuusikia wimbo huo kwenye redio na kuupenda.

"Muungano wetu usingetokea kwa namna nyingine. Tulikuwa na mipango yetu lakini Mungu alitangulia mbele yetu na ameendelea kutuongoza katika safari yetu," alisema kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mama huyo wa watoto watatu wakubwa alidokeza kwamba baada ya kukutana Guardian Angel kwa mara ya kwanza hakufikiria kwamba wangekuwa marafiki wakubwa na hatimaye kuwa mume na mke.

"Ninashukuru kuwa na wewe katika maisha yangu. Heri ya siku ya ukumbusho wa urafiki mume wangu @guardanangelglobal Nakupenda. ❤❤❤," aliandika.

Guardian Angel kwa upande aliweka wazi kuwa alimpenda mwanamke huyo wa miaka 53 baada ya kukutana naye. Katika taarifa yake, Angel alisema alipomwangalia Bi Musila aliona sifa zote anazohitaji kwa mke ndani yake.

"13/3/2020 ulinitazama ukaona supastaa. Hamu yako ilikuwa kuniona nikiwa vile ulivyoniona. Nilikutazama na kuona kila nilichotaka kwa mwanamke. Miaka mitatu baadaye sisi sote tuna kile tulichotaka," alisema.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 33 alimtaja Bi Musila kuwa mke mzuri na kukiri mapenzi makubwa kwake.