Mtoa mbegu za kiume mfululizo amefikishwa mahakamani baada ya kutuhumiwa kuwa baba zaidi ya watoto 550.
Mshtakiwa, Jonathan Jacob Meijer, 41, kutoka Hague, atafikishwa mahakamani mwezi Aprili nchini Uholanzi baada ya kufunguliwa mashtaka ya kupotosha mamia ya wanawake.
Kulingana na jarida moja la nchini Uholanzi, Wakfu wa Donorkind ulipeleka kesi mahakamani katika jaribio la kumzuia Meijer asichangie manii nyingine.
Jumuiya ya Uholanzi ya Madaktari na Magonjwa ya Wanawake kwa mara ya kwanza ilitoa tahadhari kuhusu Meijer mwaka wa 2017.
Lakini kufikia hatua hiyo, alikuwa amezaa karibu watoto 102 nchini Uholanzi baada ya kutoa mbegu za kiume katika kliniki 10.
Baadaye alipigwa marufuku katika nchi yake lakini akaamua kutoa manii nje ya nchi badala yake.
Mwanamke wa Uholanzi aitwaye Eva, ambaye mwaka wa 2018, alijifungua mtoto aliyetungwa mimba kwa mbegu za Meijer na akasema alihisi mgonjwa akifikiria madhara ambayo hatua ya Jonathan itampata mtoto wake.
Alisema: "Kama ningejua tayari ameshazaa zaidi ya watoto 100 nisingeweza kumchagua kunipa mbegu. Nikifikiria juu ya matokeo ambayo hii inaweza kuwa kwa mtoto wangu ninaumwa na tumbo langu. Kina mama wengi wamemwambia anahitaji kuacha lakini hakuna kinachosaidia. Kwa hiyo kwenda mahakamani ni chaguo pekee. Ni lazima nimlinde mtoto wangu."
Yeye na Wakfu wa Donorkind wanatumai kwamba kesi yao mahakamani itasababisha uharibifu wa mbegu za Meijer ambazo zimesalia kuhifadhiwa.
Meijer anaelezewa katika ripoti kama mwanamuziki na mkazi wa Kenya.
Ripoti zinaonyesha afya ya akili ya watoto wa wafadhili wa mbegu za kiume inaweza kuathiriwa ikiwa watagundua kuwa wana mamia ya ndugu wa kambo kwani wana wasiwasi juu ya kujamiiana na kuzaliana.