Wanandoa Esther Musila na Guardian Angel wamezungumza changamoto wanazozipitia baada ya kuweka wazi uhusiano wao kwenye mitandao ya kijamii.
Musila na Angel ambao walitokea katika halfa ya ucheshi ya mchekeshaji MCA Tricky almaarufu ‘Tricky Comedy Circuit’ walizungumza na wanablogu kwa kina huku pia Musila kwa mara nyingine akiwataka watu kujishughulisha na mambo yao na kukoma kumweka chini ya shinikizo kuhusu ni lini atapata mtoto.
“Mara ya kwanza uhusiano wetu ulipokuja mitandaoni, nilipata ugumu sana sikuwa na furaha. Jinsi umma ulichukulia huu uhusiano na zile kejeli zilizotupwa upande wetu. Lakini nahisi kwetu kusimamia kile tunakijua na ni kujijua, pia nafikiri kumesaidia watu wengi ambao wako katika uhusiano sawia na wetu,” Musila alisema.
Alitaja baadhi ya masimango kuwa ni kutukanwa na watu ambao hawamjui. Angel alisema kwamba yeye hajutii kwa sababu si yeye aliweka uhusiano wao bayana bali ni wanablogu ndio waliutoa faraghani na kuuanika hadharani.
Wengi wanaelewa kwamba uhusiano wa wawili hao ulivuma sana haswa wengi wakitilia shaka uwezo wa Musila kumzalia Guardian mtoto, ikizingatiwa kwama ana umri wa Zaidi ya miaka 50 huku mumewe akiwa na miaka 33.
Musila alijibu hilo akisema;
“Kuna swali moja ambalo huwa nauliza kila mara, mtoto wangu ana faida gani kwako wewe unauliza nitazaa lini? Utamlea au utamchunga? Si biashara yako kabisaa. Watu ni sharti wajifunze kuheshimu maisha ya watu. Wewe hunijui, huwezi kuja na kuanza kunishauri nini cha kufanya na maisha yangu. Mbona unaniambia nipate mtoto, wako? Hapana,” Musila alichemka kwa hasira.
Kwa upande wake Guradian Angel aliwashauri wanaume kukoma kuuliza mwanaume mwingine kuhusu mtoto, akiashiria kuwa wapo wanaume wengi wamekuwa wakimuuliza swali kama hilo.
“Mwanamume usiwahi uliza mwanamume mwenzako juu ya mtoto. Sababu hata wewe kama uko na wako, mama yake ndio anajua kama ni wako. Kwa hiyo unaeza kuwa hapa nje ooh huyu jamaa hapati watoto kumbe wale uko nao ni wangu,” Guardian Angel alisema akicheka.