Msani Kristoff amefunguka kwa nini anapenda kufanya collabo sana na wasanii wengi kulingansihwa na kufanya ngoma zake binafsi.
Kristoff ambaye amerejea nchini hivi majuzi baada ya kuwa kimya Marekani kwa Zaidi ya miaka miwili alijitapa kuwa ana talanta kubwa sana na kupitia talanata hiyo ya kuandika nyimbo nzuri, amewasaidia na kuwainua wasanii wengi.
“Mimi nafikiri Mungu akikupa kipaji unafaa kukitumia. Mimi nafanya vizuri na watu na ndio nikaikumbatia na imenisaidia. Nimefanya na wasanii wengi, nimewaandikia nyimbo lakini wengi huwa wanatoroka na kukuacha,” Kristoff alisema.
Msanii huyo anayejiita Mluhya wa Busia alifunguka kwamba collabo yake kubwa kabisa ya ‘Dundaing’ ambayo ilitoka mwaka 2018 ulikuwa ni wimbo wake lakini aliamua kumpa King Kaka.
Alisema kwamba anajutia kufanya uamuzi huo wa kumpa King Kaka ngoma hiyo ambayo ilifanya vizuri sana na kuwashangaza wengi.
“Wakati mwingine nahisi ile ngoma ya Dundaing nisingempa King Kaka. Kwa sababu unajua wakati unafanya ngoma hujui kama itakuwa kubwa… lakini ni mambo tu ya Mungu na kama wewe ni mbunifu utatunga ingine tu nzuri,” alisema.
Hata hivyo, alisisitiza kwamba uhusiano wake na King Kaka uko vizuri na wala hakuna bifu licha ya kujutia kumpa ngoma yake.
Kristoff alikataa kuzungumza kwa ukweli kama kuna kitu kinaendelea baina yake na King Kaka akisema “ni hadithi ndefu” huku akisema produsa Magix Enga ndiye shuhuda mkubwa na anajua kilichotokea.
Ngoma ya Dundaing iliyotoka mwaka 2018 ni moja kati ya ngoma nyingi ambazo zilibamba na kutia nakshi katika albamu ya King Kaka ya Eastlando Royalty kipindi hicho.