Mshambulizi wa Arsenal, Bukayo Saka amembwagia sifa mwimbaji wa Nigeria David Adeleke almaarufu Davido kuhusiana na albamu yake mpya ya 'Timeless'
Siku ya Jumanne, nyota huyo wa soka alichapisha screenshot ya albamu hiyo kwenye Spotify akionyesha baadhi ya nyimbo zilizopo pale.
"Davido🔥," aliandika kwenye screenshot hiyo.
Saka aliambatanisha picha hiyo na wimbo 'Unavailable' ambao ni moja ya vibao kali kwenye albamu hiyo matata.
Davido ambaye alionekana kufurahishwa sana na upendo ambao Saka alimuonyesha aliipakia picha hiyo tena kwenye ukurasa wake.
"@bukayosaka87#timeless," aliandika.
Mwimbaji huyo wa Afrobeats aliachia albamu 'Timeless' siku chache zilizopita baada ya kutangaza mwisho wa kipindi cha kumuomboleza mtoto wake Ifeanyi Adeleke ambaye alikufa maji kwenye kidibwi cha kuogelea.
Mwishoni mwa mwezi Machi, Davido katika taarifa alibainisha kuwa kila jambo lina wakati wake.
"Kuna wakati wa kila jambo. Wakati wa kuomboleza na wakati wa kupona. Wakati wa kucheka na wakati wa kucheza Wakati wa kusema na wakati wa kunyamaza," alisema.
Mwanamuziki huyo alitumia fursa hiyo kutoa shukrani za dhati kwa wote ambao walisimama naye katika kipindi kigumu cha kumuomboleza mwanae.
"Upendo wote na jumbe nilipokuwa mbali, zawadi zilizotumwa, matamasha ambayo ninyi nyote mlifanya! Ninashukuru kwa yote. Leo, nataka kuwakumbusha wote kwamba kile ambacho sasa hakina wakati, kilikuwa kipya, ni wakati wa mpya," alisema.
Wakati huohuo, alitangaza kwamba angeachia albamu yake mpya 'Timeless' baadaye mwezi huo.