Kikundi cha miziki ya injili kutoka Tanzania Zabron Singers wametangaza kuwa wapo tayari kumpokea msanii Diamond Platnumz katika Ukristo kutoka dini ya Kiislam.
Msemaji wa kikundi hicho katika mahojiano ya kituo cha redio cha Wasafi, alisema kuwa watafurahi sana iwapo msanii huyo atakubali Ukristo na kubatizwa, wakisema kuwa wako tayari kumpokea katika Usabato.
“Kitu izuri ambacho nimefurahi mimi sana ni kumuona Diamond akisoma Biblia. Nilifurahi sana na nikatamani ni bora tu aseme kuwa ameamua kuwa Muadventista Msabato, na abatizwe. Kweli sisi tutampokea na sisi Zabron tuko tayari kumlea kiroho. Tunamkaribisha kwa sababu tunampenda sana,” msemaji huyo alisema.
Diamond amekuwa gumzo la mitandaoni huku malumbano yakionekana baina ya makundi ya Ukristo na Uislamu kuhusu yeye kuonekana kanisani akinukuu Biblia siku ya Mtoko wa Pasaka licha ya kuwa ni Muislamu kindakindaki ambaye bado anasali na kufunga mwezi huu mtukufu wa Ramadhan.
Msanii huyo alilazimia kufuta chapisho kwenye Instagram yake ambalo alilipakia wiki moja iliyopita likiwa ni bango la kutangaza tukio hilo kubwa la Pasaka lililowakutanisha yeye pamoja na wasanii na wachungaji wakiwemo Rose Muhando na Christina Shusho.
Inaarifiwa kwamba Platnumz alifuta chapisho hilo baada ya makumi ya Waislamu kufika pale na kuanza kuachia meseji za “Inna lillahi wa inna ilayhi raji'un” tamko la Kiislam ambalo tafsiri yake ni “Pumzika kwa Amani” katika lugha nyepesi ya Kiswahili.
Diamond katika hotuba yake kwenye mtoko huo wa Wakristu, alizungumza kiasi na pia kunukuu baadhi ya maandiko matakatifu kutoka Biblia, jambo ambalo lilionekana kuwaghasi Waislamu.
Sheikh mmoja kwa jina Shariff amemtaka Diamond kufanya chaguo moja kama kusalia katika Uislamu na kuuheshimu au kubadili dini na kuwa Mkristo kwani hata Mungu hapendi mtu vuguvugu.
Lakini wengine wamemtetea staa huyo wa Bongo Fleva wakisema kuwa taifa lao hawana udini kwani mwisho wa siku Mungu ni yule yule mmoja ambaye dini na madhehebu yote huabudu.