logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mtoto tunaye, hatuna? Kamene Goro afunguka kuhusu kuwa mjamzito baada ya kufunga ndoa

Mtangazaji huyo aliwahi kubainisha kwamba hana mpango wa kuwahi kupata watoto.

image
na Samuel Maina

Burudani22 April 2023 - 06:43

Muhtasari


  • •Kumekuwa na uvumi kuwa kipusa huyo mwenye umri wa miaka 30 na mumewe  Dejaay Bonez wanatarajia mtoto hivi karibuni.
  • •Kamene aliwataka wanaoamini ana mimba wafike katika eneo hilo na wafinye tumbo lake ili kubaini kama amebeba mtoto.
walifunga ndoa siku ya Alhamisi, Aprili 21.

Mtangazaji Kamene Goro hatimaye amejitokeza kuzungumzia madai ya ujauzito kufuatia uvumi ulioenezwa kwenye mitandao ya kijamii.

Kumekuwa na uvumi kuwa kipusa huyo mwenye umri wa miaka 30 na mume wake mpya Dejaay Bonez wanatarajia mtoto hivi karibuni. Wawili hao walifunga pingu za maisha siku ya Alhamisi na hatua hiyo imehusishwa na ujauzito.

Huku akikanusha tetesi za kuwa na mimba, mtangazaji huyo wa zamani wa redio kwa kejeli aliwaambia wasambaza uvumi wakutane naye katika eneo la burudani mjini Nakuru ambako atatumbuiza  Jumamosi ili kuthibitisha.

"Na wenye wanasema niko na mimba, tafadhali jiskieni huru kuja Chillis  kesho (Jumamosi) usiku ili kuthibitisha," alisema kwenye Instagram.

Kamene Goro aliwataka wanaoamini ana mimba wafike katika eneo hilo na wafinye tumbo lake ili kubaini kama amebeba mtoto.

Pia aliwakejeli wasambaza uvumi hao akisema kwamba watashangaa sana kumsubiri ajifungue hivi karibuni bila kuona chochote..

"Mimi pia najiuliza, mtafanyaje ikiwa miezi michache ijayo hakuna mtoto? Aki nitawacheka," Bi Kamene alisema.

Aliongeza, "Oyaa, mume wangu Dejaay Bonez inakaa hii ndoa yetu kuna wawekezaji."

Katika siku za nyumba, mtangazaji huyo wa zamani aliwahi kubainisha kwamba hana mpango wa kuwahi kupata watoto.

Kamene Goro alifunga pingu za maisha na mpenzi wake David Pyper almaarufu Deejay Bonez siku ya Alhamisi katika harusi ya faragha iliyohudhuriwa na wanafamilia kadhaa na marafiki wachache wa karibu.

Mbunge wa eneo la Lang’ata, ambaye ni rafiki wa karibu sana na mtangazaji mwenza wa zamani wa Kamene Goro alishiriki picha na video za tukio zima kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuwapongeza wawili hao.

"Mapenzi ni kitu kizuri! Hongera sana dada yangu @kamenegoro na @deejaybonez254 kwenye siku ya harusi yenu! Nawapenda wadau," alisema.

Baadaye, muundaji maudhui Andrew Kibe aliibua malalamishi dhidi ya mwenzake  wa zamani huyo kwa kutomwalika kwenye harusi hiyo.

Akizungumza wakati wa kipindi cha moja kwa moja siku ya Alhamisi jioni, Kibe alilalamika kuwa mtangazaji mwenzake huyo wa zamani hakumwalika kwenye hafla hiyo  licha ya kufanya naye kazi hapo awali.

"Mtu tulifanya kazi na yeye bro. Mtu nilienda nikamtetea mshahara nikasema tafadhali mpatie nyongeza," Kibe alisema.

Mtumbuizaji huyo ambaye kwa sasa anaishi Marekani aliweka wazi kwamba kutoalikwa kwenye harusi hiyo kulimvunja moyo.

"Naweza anza kutoa machozi hapa. Mbona hukunitumia mwaliko wa harusi," alilalamika.

Kibe pia alishangaa kwa nini kipusa huyo mwenye umri wa miaka 30 alimchagua mcheza santuri kuwa mwenzi wa maisha.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved