Hamisa Mobetto afunguka kuhusu ndoto ya kuolewa, hamu ya kuzaa watoto watano

"Sasa hivi sizai bila kuoelewa. Ningekuwa nimeolewa ningekuwa nimejaza nyumba," Hamisa alisema.

Muhtasari

•Hamisa alisema anatazamia kuzaa watoto wengine watatu pindi baada ya kupata mwanaume wa kufunga ndoa naye. 

•"Kitambo nilikuwa siamini katika ndoa. Sasa najua nataka lakini sio sasa hivi. Tunasubiria wakati wa Mungu," alisema.

Image: INSTAGRAM// HAMISA MOBETTO

Mwanamitindo na mwimbaji mashuhuri kutoka Tanzania Hamisa Mobetto amefunguka kuhusu mipango yake ya kifamilia.

Katika mahojiano na PMTV, mama huyo wa watoto wawili aliweka wazi kwamba anatazamia kuolewa na kuongeza watoto.

Alisema anatazamia kuzaa watoto wengine watatu pindi baada ya kupata mwanaume wa kufunga ndoa naye. 

"Zamani nilitaka watoto saba, lakini sasa hivi nataka watano. Tayari niko na watoto wawili, nimebakisha wengine watatu. Wakati nikioelewa, mwaka wa kwanza napata mtoto mwingine," Mobetto alisema.

Mpenzi huyo wa zamani wa staa wa bongo Diamond Platnumz aliweka wazi kwamba hatapata mtoto mwingine kama bado hajajitosa kwenye ndoa.

"Sasa hivi sizai bila kuoelewa alisema," alisema.

Alisema ndoto yake ya kupata watoto wengi ilitokana na kuwa alizaliwa pekee yake katika familia yao.

"Mimi ni mtu ambaye anapenda watoto wengi. Nimezaliwa pekee yangu kwa hivyo mimi nataka niwe tofauti. Ningekuwa nimeolewa ningekuwa nimejaza nyumba," alisema.

Hamisa Mobetto aliweka wazi kuwa sasa amebadili msimamo wake kuhusu ndoa. Alibainisha kwamba hapo awali hakuamini katika ndoa ila sasa hali imebadilika na anatamani kuoelewa katika siku zijazo.

Hata hivyo, alibainisha kuwa kuna malengo ambayo anatazamia kutimiza kabla ya kupiga hatua hiyo kubwa ya maisha.

"Ndoto za ndoa zipo, lakini sio sasa. Kuna malengo ambayo nimejiwekea nataka nitimize kabla sijaoelewa. Niko karibu kutimiza, imebaki kidogo tu. Nikikamilisha hiki cha mwisho nitakuwa tayari kuwa mke wa mtu," alisema.

Aliongeza, "Kitambo nilikuwa siamini katika ndoa. Sasa najua nataka lakini sio sasa hivi. Tunasubiria wakati wa Mungu."

Hamisa Mobetto bila shaka ni mmoja wa wanawake maarufu na wanaofuatiliwa zaidi nchini Tanzania na kote  Afrika Mashariki.  Amejikita katika mitindo, biashara ya nguo na pia ni mwanamuziki wa muda.

Pia ni mama wa watoto wawili, Fantasy Majizzo na Deedaylan Abdul Naseeb ambao amezaa na wapenzi wawili wa zamani tofauti. Fantasy ambaye ni mtoto wake na mjasiriamali Francis Ciza Majizzo alizaliwa mwaka wa 2015 ilhali Dylan ambaye anaaminika kumzaa na Diamond Platnumz alizaliwa 2017.

Mwanamitindo huyo sasa ameweka wazi kwamba anatamani kuolewa na mwanaume kutoka eneo la Pemba, Tanzania.