Mke wa mchungaji wa Bungoma mwenye utata Eliud Simiyu almaarufu Yesu wa Tongaren, nabii Benjamin amewakosoa wafuasi wa mchungaji Paul MacKenzie kwa kukubali kushurutishwa kufunga hadi kufa ili kukutana na Yesu.
Akizungumza katika mahojiano, nabii Benjamin alisema waumini hao hawakufaa kujikandamiza ili mradi tu kukutana na Yesu Kristo kwani kulingana naye, Yesu yuko hapahapa duniani na ana makao yake katika kaunti ya Bungoma.
"Yesu hayuko mbinguni, Yesu ndiye huyu tumekaa naye duniani," Benjamin aliambia The Great Tv.
Alitoa wito kwa wale ambao wameokolewa kutoka kwa ibada hiyo kufunga safari hadi Bungoma ili kukutana na 'Yesu' uso kwa uso.
"Wawekwa kwa magari na mabasi wakuje hapa kwa Yesu waonane na Yesu mwenyewe uso kwa uso. Kwa maana leo hii tuko na Yesu hapa duniani ndiye huyu mnamuona kwa vyombo vya habari. Tuko na baba Mungu," alisema.
Benjamin alidai wafuasi wa mchungaji huyo mwenye utata waliopoteza maisha kwa kufunga hadi kifo wameishia jehanamu.
Bw Simiyu pia alitoa wito kwa waumini ambao wameokolewa kuelekea Bungoma ili kukutana naye ili awape mwelekeo mwema. Aliwahurumia na kumuomba Mwenyezi Mungu awasaidie warejeshe afya njema ambapo baada ya hapo amejitolea kuwaongoza katika njia sahihi ya kwenda mbinguni.
"Kwa wale ambao wameokolewa, naomba Mungu awatendee na awarejeshe afya maana huenda wako na madhaifu katika viungo vya miili yao. Mungu akiwapa afya, ombi langu ni kwamba wajue Yesu yumo humu duniani na amekuja kuhubiri injili kwa viumbe wote duniani. Hivyo ndivyo walivyo," alisema.
Aliweka wazi kuwa hakumjua mchungaji MacKenzie hadi alipokuja kujulikana hivi majuzi kufuatia madai mazito dhidi yake. Hata hivyo alibainisha kuwa hatamhukumu kuhusiana na madai dhidi yake.
Paul Mackenzie, ambaye ni kiongozi wa Kanisa la Good News International, anakabiliwa na makosa makubwa ya mauaji, kushauri na kusaidia watu kujiua, utekaji nyara, kuendeleza itikadi kali, mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya binadamu, ukatili wa watoto, utapeli, ulaghai miongoni mwa mengine.
Ijumaa, timu ya mashtaka inayoshughulikia kesi dhidi yake iliomba mahakama kuruhusu serikali kumzuilia mshukiwa, na washtakiwa wenzake, kwa siku 90 zaidi ili kuruhusu kukamilika kwa uchunguzi.