Saa chache baada ya kuvishwa pete ya uchumba, Nicah the Queen ameibuka akidai kwamba hana uhasama wowote na Dr Ofweneke, ambaye ni baba wa watoto wake na mume wake wa zamani.
Nicah alipakia video ya enzi hizo wakiwa wanaigiza na Ofwekene kwenye simulizi na Maisha Magic ambapo walikuwa wanazungumzia maisha ya familia yao changa.
Katika video hiyo, wawili hao enzi za mapenzi Ofweneke alionekana akimwambia kwamba katika nyumba ni yeye tu alikuwa anafaa kuwa miandaoni, wakizungumzia kuhusu watoto wao wawili miongoni mwa mambo mengine ya kujenga familia.
Nicah aliisindikiza video hiyo na maneno ya kuwatumbua wale wanaoshabikia bifu na kunyoosha maelezo kwamba yeye hana uchungu kwa kuachwa na Ofweneke.
“Nilichagua mazingira yenye afya na mazuri kwa ajili ya Baba watoto wangu, watoto wangu na mimi.......Nilichagua amani badala ya uchungu na mazungumzo ya heshima badala ya matusi na kwa taarifa yako nitamtag na kumpost EX wangu nikipendaπ ππ Mimi sio EX mwenye uchungu kama ndivyo mlivyotarajia,” Nicah aliwazima wenye husda.
Msanii huyo wa injili alisema hayo baada ya kufichua kwamba alilazimika kukataa posa za ndoa 12 kutoka kwa wanaume tofauti baada ya kuachana na Ofweneke mwaka 2017.
Nicah alivishwa pete ya uchumba na mpenzi wake wa muda DJ Slahver katika hafla ya kipekee ambapo alifungwa macho na kuongozwa hadi kwenye zulia la waridi ambako Slahver alikuwa amepiga goti akimsubiri na pete mkononi.