Mwigizaji mkongwe Fridah Kajala kwa mara ya kwanza kupitia kipindi cha uhalisia amefichua kwamba kwa kipindi kimoja bintiye wa pekee Paula Kajala aliwahi bugia simu kwa lengo la kijitoa uhai.
Katika kipindi hicho kipya cha uhalisia cha Paula na mamake ambacho kinapeperushwa kupitia runinga ya Zamaradi kwenye king’amuzi cha Azam kwa jina Behind the Gram, Kajala alisimulia kuwa kilikuwa ni kipindi kigumu sana huku akijuta kuendekeza sana ustaa na kumtelekeza bintiye ambaye alifikia hatua ya kutaka kujiua kwa sababu ya kijihisi kutopata mapenzi dhati ya mzazi.
“Hamna mtu ambaye anajua kwamba kuna kipindi Paula alitaka kujiua kwa kunywa sumu. Naona kabisa kwamba nilijali mapenzi kuliko mtoto wangu. Kuna vitu ambavyo navifanya kupitia kwa ujinga wangu najisikia vibaya lakini sina cha kufanya,” Kajala alisema huku machozi yakimlengalenga.
Alisema kuwa mtu pekee anayemuelewa ni bintiye Paula huku binti huyo naye akisema kwamba maisha ya kuwa kwenye mwanga wa mitandao ya kijamii muda wote yamewagharimu kwa kiasi kikubwa kwani kila mtu anafikiria kwamba wao hawana maisha yao ya faraghani.
Wiki mbili zilizopita akiwa nchini Kenya, mwigizaji huyo kwa mara ya kwanza alitoa mwanga kuhusu kilichokwamisha uhusiano wake na aliyekuwa mpenzi wake msanii Harmonize.
Kulingana na Kajala, aliamua kumpa Harmonize nafasi na muda wa kujifurahisha na kujivinjari maisha ya ujana kwani alihisi msanii huyo bado ni mchanga sana na hajakamilisha raha za ujanani na kuwa naye kulikuwa kwa kiasi Fulani kunakwamisha hilo kwake.