Sonko asherehekea maendeleo ya kijana aliyechukua kuwa mwanawe baada ya mamake kuuawa Likoni

Gift Osinya alichukuliwa na Sonko baada ya kunusurika katika shambulizi la kigaidi katika kanisa la Likoni mnamo Machi 3, 2014.

Muhtasari

•Gift Osinya anasherehekea siku yake ya kuzaliwa ya 22 na gavana huyo wa zamani wa Nairobi amemsherehekea kwa njia maalum.

•Mike Sonko alibainisha kwamba kijana huyo mwenye umri wa miaka 22 ni baraka kubwa katika familia yake.

Image: TWIITTER// MIKE SONKO

Aliyekuwa gavana wa kaunti ya Nairobi Gideon Kioko Mbuvi almaarufu Mike Sonko amemsherehekea mtoto wake wa kulea, Gift Osinya mnamo siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwake.

Gift Osinya ambaye alichukuliwa na Mike Sonko takriban miaka kumi iliyopita baada ya kuokolewa kutoka kwa shambulio la Al shabaab katika eneo la Likoni, kaunti ya Mombasa anasherehekea siku yake ya kuzaliwa ya 22 na gavana huyo wa zamani amemsherehekea kwa njia maalum.

Katika taarifa yake ya siku ya Alhamisi, mfanyabiashara huyo alikumbuka jinsi shambulio hilo baya lilivyomwacha mama yake Osinya akiwa amefariki na jinsi wakosoaji  wake walivyoibua madai kwamba alikuwa akijipigia debe tu alipomkaribisha kijana huyo na mdogo wake nyumbani kwake.

"Umekua haraka sana na sasa wewe ni mwanafunzi wa mwaka wa 2 katika Chuo Kikuu cha Kikristo cha Scott's. Hata hivyo, miaka kumi iliyopita idadi kubwa ya wakosoaji wangu walifikiri kwamba nilikuwa nikicheza PR na wewe tu na mdogo wako Baby Satrin ambaye ulimwokoa kutokana na mvua ya  risasi kutoka kwa magaidi wa alshabab ambao walimuua marehemu Mama yako, nakumbuka vizuri sana kipindi chako cha kilio wakati wa siku ngumu za kwanza ulipojiunga nasi kama familia," Sonko alisema kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Gavana huyo wa zamani aliambatanisha ujumbe wake na picha zilizoonyesha maendeleo makubwa katika maisha ya Osinya kutoka alipookolewa hadi sasa ambapo ni mwanafunzi wa chuo kikuu.

"Leo nawaambia walimwengu kuwa shetani ni mwongo maana Mungu alifuta machozi yako kwa furaha na upendo tele," alisema.

Mike Sonko alibainisha kwamba kijana huyo mwenye umri wa miaka 22 ni baraka kubwa katika familia yake.

Huku akimtakia heri ya siku ya kuzaliwa, mwanasiasa huyo alimtakia Osinya baraka na uongozi wa Mola maishani.

"Naomba Mungu wa Danieli, Meshack na Abednego aliyeokoa maisha yako, na ya mdogo wako, atembee nawe kila wakati," alisema.

Gift Osinya alichukuliwa na Sonko baada ya kunusurika katika shambulizi la kigaidi katika kanisa la Likoni mnamo Machi 3, 2014.

Watu sita walifariki katika shambulio hilo, akiwemo mamake Satrin Osinya ambaye alikuwa na umri wa miezi 18.