Alidaiwa kuwa mpenzi wa mwanasosholaiti Sharifa Sharon Wambui almaarufu Manzi wa Kibera amevunja ukimya baada ya kutengana.
Katika mahojiano na Nicholas Kioko siku ya Ijumaa, mzee huyo mwenye umri wa miaka 66 alithibitisha kuwa mahusiano yao ya miezi michache yamefika kikomo na kubainisha kuwa jambo hilo limemuacha amevunjika moyo.
Alisema mwanasosholaiti huyo hajakuwa akipokea simu zake hivi majuzi licha ya mipango yao ya ndoa kukaribia kukamilika.
"Sijui kwa nini amenitoroka hivyo na tulikuwa tunapanga harusi nzuri. Tulipima nguo yake sasa nashindwa ni nini mbaya na yeye," alilalamika.
Aliongeza, "Tulikuwa tupange mpango kidogo ya harusi yetu. Sasa nikipiga simu hachukui. Sijaskia kutoka kwake."
Mzee huyo alisema anashuku kwamba mwanasosholaiti huyo angeweza kumtoroka baada ya pesa zake kuanza kupungua.
"Pengine aliona pesa yangu imeenda chini kidogo. Kwa kweli ata mimi sipendelei mambo yangu na yeye sasa," alisema.
Aliweka wazi kwamba hakuwahi kumkosea Manzi wa Kibera kiasi cha kumfanya achukue hatua ya kukatiza mahusiano yao.
Aidha, alisisitiza kwamba mapenzi yao yalikuwa ya kweli bali sio kuigiza kama jinsi ambavyo wengi wamekuwa wakidai.
"Harusi tulikuwa tumepanga ifanyike mwezi ujao.. Amenipeleka hasara kwa sababu nimeshapima nguo yake," alisema.
Alisema iwapo mwanasosholaiti huyo kutoka Kibera hatachukua simu yake, basi yuko tayari kuachana naye na kusonga mbele.
Mwanasosholaiti Manzi wa Kibera alitangaza kutengana na mchumba huyo wake wa miaka 66 siku ya Alhamisi baada ya wawili hao kufurahia mahusiano kwa miezi kadhaa.
Kwenye instastori zake, mwanasosholaiti huyo aliyeonekana kujawa na huzuni alitangaza kuwa yeye na mzee hawako pamoja tena.
"Mimi na mzee hatuyuko pamoja tena," alisema Manzi wa Kibera na kuambatanisha ujumbe wake na emoji za huzuni.
Haya yanajiri wiki chache tu baada ya mrembo huyo kutoka mtaa wa Kibera kudaiwa kuvishwa pete ya uchumba na mzee huyo.
Katika video zilizovuma kwenye mitandao ya kijamii, mwanasosholaiti huyo asiyepungukiwa na drama alionekana akiwa ameandamana na mchumba wake kabla ya mzee huyo kupiga magoti na kumuomba wafunge ndoa. Makumi ya watazamaji kisha walisikika wakimtia moyo kukubali ombi hilo la ndoa.
"Sawa, nishasema ndio!" alisikika akimwambia mpenzi huyo wake baada ya muda mfupi wa kufikiria na kuzingatia.
Baada ya kukubali, mzee huyo aliyekuwa amevalia kapura nyeupe na koti nyeusi alionekana akimvisha pete ya uchumba.
Watazamaji waliweza kusikika wakimsihi mwanasosholaiti huyo kumbusu mchumba wake na wanaonekana kutii ombi.