Malkia wa muziki wa Kenya Nadia Mukami amefunguka kuhusu utamaduni wa wakwe zake ambao ulimshtua wakati alipowatembelea.
Akizungumza kupitia ukurasa wake wa Instagram siku ya Ijumaa, msanii huyo mwenye umri wa miaka 26 alisema alishangaa kuona wanawake wakipiga magoti wakati wakiwasalimia wazee na kuwapa chakula na vinywaji waume zao.
"Nilipoenda kwa shagz ya Arrow Bwoy niliona wakwe kutoka upande wake wakipiga magoti wakati wa kusalimiana na wazee au wakati wa kuwapakulia waume wao, hiyo ilikuwa tamaduni ya kushtua kwangu ya Uganda," Nadia alisema.
Mama huyo wa mtoto mmoja aliambatanisha taarifa hiyo na video yake akiiga utamaduni wa wakwe zake kuhusu jinsi ya wanawake kuwatendea waume zao. Katika video hiyo, alionekana akiweka chakula kwenye sahani kisha kumpa maji mume wake Arrow Bwoy huku akiwa amepiga magoti.
"Ulipata mshtuko gani wa tamaduni ulipokutana na wakwe zako," aliwauliza mashabiki wake kwenye Instagram.
Nadia na mzazi mwenzake Arrow Bwoy ambao wote ni wanamuziki wanaendelea kuipigia debe EP yao ya pamoja ya 'Love &Vibes. EP hiyo yenye nyimbo walizofanya pamoja inatarajiwa kuachiwa tarehe 2 Juni.
Mastaa hao wawili wamekuwa kwenye mahusiano kwa muda mrefu na hata wamebarikiwa mtoto mvulana pamoja, Haseeb Kai.
Desemba mwaka jana hata hivyo, Nadia alikuwa ameibua wasiwasi kuhusu mahusiano yao huku akidokeza utengano.
Katika taarifa yake kwenye mtandao wa Instagram, alisema walimaliza uhusiano wao kitambo lakini wakachagua kuficha.
Wakti huo alieleza kwamba hawezi kuendelea kusema uwongo kuhusu hali halisi ya uhusiano wao.
"Ili tu kuwafafanulia watu ili wabook Arrow Bwoy na mimi. Nimeishiwa na uwongo. Hatujakuwa pamoja kwa muda, tuliachana," aliandika.
Mwezi Machi mwaka huu, Arrow Bwoy hata hivyo alikana kuwahi kutengana na mzazi huyo mwenzake kama alivyodai mwaka jana.
Akizungumza kwenye mahojiano, baba huyo wa mtoto mmoja alisema Nadia bado ni mpenzi wake na mama wa mtoto wake.
“Sijawahi kutoa taarifa na wala sijawahi kuondoka wala kuachwa na mtu, kwanza nijuavyo mimi Nadia ni mama wa mtoto wangu na mpenzi wangu,” alisema.
Arrow Bwoy ni mzaliwa wa eneo la Magharibi mwa Kenya ilhali mke wake Nadia Mukami ametokea eneo la kati mwa Kenya.