Mwimbaji wa muziki wa dancehall kutoka Ghana, Francine Koffie almaarufu Fantana amemjibu vikali mzazi mwenza wa Diamond Platnumz, Zari Hassan baada ya kumshambulia kutokana na uhusiano wake na staa huyo wa Bongo.
Katika jibu lake kwa kwenye Instagram, Fantana aliibua madai kwamba mwanasosholaiti huyo hudanganya kuhusu yeye kuwa bilionea.
"Je, unajua ni nini maana ya kuwa bilionea? Nadhani wanapeana hadhi ya bilionea bure tu. Mtu tafadhali ampe huyu mwanamke dawa yake," Fantana alimwambia Zari Hassan kupitia kwenye Instastori zake.
Mwanamuziki huyo wa Ghana mwenye umri wa miaka 25 ambaye alizaliwa na kukulia Marekani aliendelea kushambulia Zari akidai alifanyiwa ukarabati wa mwili wake ili aonekane mchanga na wa kuvutia zaidi.
Pia alimshtumu mwanasosholaiti huyo kwa kughushi maisha yake ya kifahari na kudai ameolewa na kijana mdogo.
"Taaluma iliyofeli? Ulifanikiwa nini ukiwa na miaka 25? Uliweza kupata iPhone, ukanunua mtandao na ukajenga maisha ya uwongo.... sasa umeolewa na kijana wa shule ya upili" Fantana aliendeleza mashambulizi.
Alidokeza kuwa mama huyo wa watano anamuona kama tishio kubwa kwake.
Hapo awali, Zari alimkosoa mzazi mwezake, Diamond kwa madai ya kumwambia Fantana maneno ya uwongo kuhusu uhusiano wao.
Katika tukio moja kwenye filamu ya uhalisia iliyoachiwa siku ya Ijumaa, Young, Famous and African sehemu ya pili, Diamond Platnumz alisikika akimwambia mshikaji wake mpya, Francine Koffie almaarufu Fantana kutoka Ghana kwamba mpenzi wake wa zamani Zari Hassan alitaka mtoto wa tatu naye.
Staa huyo wa Bongo alidai kuwa Zari alitaka kupata mwanamke mwingine wa kumbebea mtoto wao wa tatu.
"Zari alitaka mtoto mwingine nami. Alitaka kupata mtu wa kumzalia mtoto," Diamond alimwambia mwimbaji huyo wa Ghana.
Katika majibu yake yaliyojaa machungu siku ya Jumamosi, Zari Hassan alikanusha madai kuwa bado anampenda mwimbaji huyo wa Tanzania mwenye umri wa miaka 32 na kwamba aliomba kuzaa naye mtoto mwingine.
Mwanasosholaiti huyo alidai kuwa Diamond ndiye amepata ugumu wa kusonga mbele baada ya. mahusiano yao kuvunjika.
"Sikutaki, sijapagawa na wewe, kwa kweli ni kinyume chake. Umepagawa na mimi, inaonekana huwezi kupata wa kuchukua nafasi yangu. Utakuja mbio kama duma nikikuita urudi. Ninaelewa tu kwa sababu ya heshima kwa ajili ya watoto," Zari alisema.
Mwanasosholaiti huyo mwenye umri wa miaka 42 alimshutumu Diamond kwa kuwaruhusu wapenzi wake wadogo kutomheshimu ili tu kulala nao, mashambulizi ambayo yalionekana kuelekeza kwa Fantana.
Pia alifichua kuwa madai ya staa huyo wa Bongo dhidi yake yalisababisha mgogoro katika ndoa yake mpya na Shakib.
"Mimi ni mwanamke aliyeolewa hivi sasa na madai yako hayakukaa vizuri na ndoa yangu. Shoo kuhariri tu sehemu zinazowafaa ni upuuzi. NILIWEKA WAZI MIMI NIKO NA MTU SASA, siwezi kuzaa na wewe," Alisema.
Zari Hassan pia alimshtumu mpenzi huyo wake wa zamani kwa kupenda kutafuta kiki sana na kujinufaisha na drama.
Kutokana na hayo, aliweka wazi kuwa uhusiano wao hautakuwa sawa tena na kubainisha kuwa anaweza kujisimamia mwenyewe.