Msanii wa Mugithi DJ Fatxo kwa mara ya kwanza amezungumza kwa njia ya kipekee kuhusu sakata ambalo limekuwa likimuandaman katika kifo cha aliyekuwa mbunifu wa mapambo Jeff Mwathi.
Fatxo akizungumza katika kipindi cha Radio Jambo na mtangazaji Massawe Japanni, alisema kuwa walikutana na marehemu katika duka la kuuza viatu na alikuwa ni kijana mzuri ambaye alikua na kuwa rafiki wa karibu.
Fatxo alisema kuwa anashangaa ni kwa nini watu wengi wamekuwa wakimshuku kuwa muuaji wa Mwathi, wakati anajua kuwa yeye hangeweza kuua.
“Mimi sijishuku kwa sababu siwezi ua, Jeff alikuwa rafiki yangu na sioni kwa nini ningeweza kumuua, ni kijana mdogo tu,” Fatxo alifunguka.
Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa msanii huyo wa Mugithi kuzungumza hadharani kwenye kituo cha redio, wiki moja baada ya kuondolewa mashtaka dhidi ya mauaji ya Mwathi ambaye alifariki katika nyumba anakoishi Fatxo mtaani Kasarani.
Fatxo alieleza kwamba Jeff alijipata kwa nyumba yake siku ambayo umauti ulikuja kumpata na alikuwa anapanga kukutana naye ili kumwelezea wazo lake la kufanyiwa ubunifu katika biashara yake ya kufunza wacheza santuri, DJs.
Jeff alimtafuta WhatsApp na akamtaka wakutane na hivyo ndivyo Faxto walikutana naye akiwa na jamaa mwingine kwa jina Kinuthia.
Huo ndio ulikuwa mwanzo wa mizunguko na misele yao kutoka klabu moja hadi nyingine hadi wakalewa na akaamua kumrudisha nyumbani kwake ili alale.
Wiki jana baada ya Faxto kupitia kwa mawakili wake kuiandikia DPP kuhusu kutaka majibu ya uchunguzi wa mauaji ya Jeff, DPP walitoa ripoti hiyo na kumtolea mashtaka yote ambapo Faxto alisema alikuwa amechafuliwa jina kwa kiasi kikubwa.