•Familia ya marehemu ilithibitisha habari za kuhuzunisha za kifo chake siku ya Jumamosi kupitia akaunti yake rasmi ya Tiktok.
•Siku chache zilizopita, marehemu alitengeneza video akielezea kuwa alikuwa kimya kwani alikuwa akipambana na ugonjwa.
Mtumbuizaji maarufu wa Tiktok wa Kenya, Shosh wa Kinangop amefariki.
Familia ya marehemu ilithibitisha habari za kuhuzunisha za kifo chake siku ya Jumamosi kupitia akaunti yake rasmi ya Tiktok.
Video ya ajuza huyo akiwa amepumzika kwenye kiti cha magurudumu huku akionekana kutojisikia vizuri ilichapishwa kwenye akaunti yake Jumamosi jioni.
“Rest in peace shosh,” ilisomeka taarifa fupi iliyoandikwa kwenye video hiyo.
Sauti ya wimbo maarufu Tanzania Blessing Voice 'Tazama Wanavyoomboleza Kwa Uchungu' iliambatishwa kwenye video hiyo kuashiria hali ya huzuni iliyoikumba, sio familia yake tu, bali jamii nzima ya Tiktok ya Kenya.
Maelfu ya wanamitandao hasa Wakenya watumizi wa Tiktok wameendelea kumuomboleza shabiki huyo sugu wa klabu ya Manchester United ambaye kwa muda mrefu alizipasua mbavu zao kwa video zake za kuchekesha.
Maryam:Ni siku mbaya sana kwetu kama mashabiki wa Man u, tumepoteza kombe la FA na shabiki mkubwa...rip shosh.
Chief GKW: Pumzika kwa amani Shosh, nilikuwa na wakati mzuri nitazama video zako.
Ellyummy: Tumempoteza mfuasi mkubwa wa Man U... Rest Easy Shosh😭
BECKY BELLA: Shosh wetu ameenda. Hapana, haiaminiki, roho yake ipumzike kwa amani. Alikuwa na furaha wakati wote.
Carolselle: Ghaaaai oooooooh tulivyokupenda shosh ila Mungu alikupenda zaidi pumzika 💔
Kifo cha nyanya huyo mzee kimekuja siku chache tu baada ya wanamitandao kuibua wasiwasi kuhusu aliko baada ya kugundua kuwa hakuwa ametengeneza video yoyote kwa muda, jambo ambalo halikuonekana kuwa la kawaida.
Siku chache zilizopita, marehemu alitengeneza video akielezea kuwa alikuwa kimya kwani alikuwa akipambana na ugonjwa.
"Watu wangu, ni kugonjeka niligonjeka. Lakini msione kama nimepotea, sijapotea. Nikipona tutaonana, Mungu ni mwema nitapona," Shosh wa Kinangop alisema kwenye video iliyochapishwa kwenye akaunti yake.
Mamia ya wanamitandao walikuwa wamejitokeza kumatakia ajuza huyo mchekeshaji afueni ya haraka. Kwa bahati mbaya, ugonjwa huo haukumruhusu kuendelea kuwaburudisha wengi kwa muda zaidi. Roho yake ipumzike kwa amani.