Msanii kinara katika kundi la Sauti Sol, Bien amefichua jinsi kundi hilo lilivyoanzishwa takribani miongo miwili iliyopita.
Akizungumza kwa njia ya kipekee katika maandalizi ya shoo kubwa ya Stanbic Yetu Festival inayoandaliwa na kampuni ya Radio Africa kwa kushirikiana na benki ya Stanbic, Bien alisema kuwa kipindi hicho wakiwa vijana chipukizi walikuwa wanajaribu kujinafasi kwenye muziki kwa kuimba ukarabati wa nyimbo za kundi la Boyz II Men kutoka Marekani.
“Ahsante sana kwa kutupa nafasi ya kipekee kutumbuiza na wanamuziki ambao tumekuwa tukiwaangalia kama kielelezo. Sijui kama mnajua hili lakini Sauti Sol iliasisiwa kwa kuimba ‘cover’ za nyimbo za Boyz II Men. Taaluma yetu ilichochewa na Boyz II Men kwa muda mrefu,” Bien alisema.
Msanii huyo alisema kuwa kushuhudia kundi la Boyz II Men wakitumbuiza katika udongo wa Kenya kwa mara ya kwanza kwa Zaidi ya miaka 30 tangu walipokuwa wanavuma nchini ni hatua kubwa kwa wasanii wa Kenya kupata kujifunza jambo moja kimuziki.
Boyz II Men watakuwa wanatumbuiza Jumamosi katika tamasha la Stanbic Yetu Festival itakayoandaliwa kwenye uwanja wa Uhuru Gardens jijini Nairobi na kundi la Sauti Sol litakuwa moja ya wasanii wa Kenya ambao watapata nafasi adimu ya kutumbuiza nao.
Tamasha hilo ambalo linaandaliwa kwa mara ya pili linafadhiliwa na benki ya Stanbic kwa ushirikiano na kampuni ya Radio Africa Group.
Wakenya wengi walishambulia tiketi za kuwa miongoni mwa watakaoandikisha historia kushuhudia Boyz II Men wakitumbuiza na Sauti Sol katika kile ambacho kimetajwa kuwa huenda ikawa ndio mara ya mwisho kabisa kwa kundi hilo la Kenya kutumbuiza pamoja kwani tayari wameshatangaza kuchukua likizo ili kila mmoja kujishughulisha na masuala ya kwake binafsi.