Mwezi Juni mwaka 2020 wakati mke wa meneja wa Diamond Platnumz, Babu Tale alifariki, msibani ndio kulikuwa mara ya kwanza wasanii Diamond na Harmonize kukutana uso kwa uso, baada ya takribani mwaka mmoja wa kutoonana kutokana na Harmonize kuondoka WCB kwa njia ya shari mwishoni mwa mwaka 2019.
Wasanii hao wawili licha ya kuwa katika tukio ambalo mara nyingi huwakutanisha watu mahasimu na hata kuwafanya kuzika tofauti zao, wao hawakusalimiana na muda wote walikuwa wamevimbiana makaburini.
Miaka mitatu baadae, sasa meneja huyo Babu Tale amefunguka kuhusu tukio hilo na kusema kwamab kuwaona Harmonize amevimbiana na Diamond na meneja mwingine Sallam SK kulimuumiza sana.
Tale alisema kuwa alifurahia na kuipenda video ya Harmonize akisalimiana na SK Zanzibar na kusema ni tukio zuri kuliko lile ambalo aliliona kwenye msiba wa mke wake.
“Video ya Harmonize akikutana na Sallam Zanzibar mimi nimeipenda. Sikupendezwa ile ya wakati wakiwa kwenye msiba wa mke wangu kule wakavimbiana. Hawakusalimiana. Yaani kwa kuwa sikuwa na uwezo wa kuongea wala kufanya mahojiano yoyote, muda ule nikawaangalia tu. Sikupenda. Mimi nasalimiana na Harmonize siku zote, hata yeye akinikuta ananisalimia bosi shikamoo marahaba freshi…” Babu Tale aifunguka.
Mbunge huyo alitoa maoni kwamba kama kuna mtu ambaye anatarajia kabisa kuwaona Diamond na Harmonize wakimaliza ugomvi wa basi ni yeye, kwani hakuna kitu kizuri kama watu kupendana.
“Hakuna kitu kizuri kama vita kuisha. Diamond hawezi kuwa na vita ya kibinafsi na Harmonize. Utaratibu aliopita nao Harmonize ndio utaratibu ambao Rayvanny amepita, ila kwa nini Diamond aseme anamchukia huyo na si huyu wa pili? Uongo, ni maneno tu ya watu yanatengenezwa na kuna mahali yanafika watu wanaamini ni ukweli,” Tale alieleza.
Tale alisema kuwa kwa sasa hawawasiliana na Harmonize kwa sababu biashara ilishaisha lakini haimaanishi kwamba ushikaji ulikatika, au uadui uliingia.