Mwimbaji Anjella avunja kimya kuhusu Kajala kuhusika katika kutimuliwa kwake Kondegang

Msanii huyo wa zamani wa Kondegang aliweka wazi kwamba hakuwahi kuwa na uhusiano wa karibu sana na Kajala.

Muhtasari

• Anjella aliweka wazi kuwa hafikirii kuwa Kajala ndiye aliyesababisha kukatizwa kwa mkataba wake na lebo hiyo.

•Alisema alikuwa akiwasiliana na muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 40 wakati tu hitaji la kikazi  lilipotokea.

Anjella na Harmonize
Image: HISANI

Aliyekuwa msanii wa Konde Music Worldwide, Angelina Samson almaarufu Anjella amejibu madai kuwa muigizaji Frida Kajala Masanja ndiye aliyemfanya yeye na wasanii wengine waliokuwa wamesainiwa na lebo hiyo kutimuliwa.

Akizungumza kwenye mahojiano na Millard Ayo, Anjella aliweka wazi kuwa hafikirii kuwa mpenzi huyo wa zamani wa bosi wa Kondegang Harmonize ndiye aliyesababisha kukatizwa kwa mkataba wake na lebo hiyo.

"Sidhani, mimi sidhani," Anjella alijibu baada ya kuulizwa ikiwa muigizaji huyo mkongwe alihusika katika kutimuliwa kwake.

Malkia huyo wa muziki mwenye sauti nzuri aliweka wazi kwamba hakuwahi kuwa na uhusiano wa karibu sana na Kajala.

Alisema alikuwa akiwasiliana na muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 40 wakati tu hitaji la kikazi  lilipotokea.

"Kusema ukweli nilikuwa sina stori sana naye. Ilikuwa kukiwepo na jambo, naenda namwambia. Kama ni jambo fulani namwambia. Lakini hakukuwepo na yale mazoea ya kusema mnawasiliana labda," alisema.

Wakati wa mahojiano hayo, Anjella alibainisha wazi kwamba lebo ya Kondegang ndiyo iliyovunja mkataba wake nao.

Alisema lebo hiyo inayoendeshwa na Harmonize ilitaja kushindwa kwake kuwasilisha kazi kama ilivyokuwa imekubaliwa kwenye mkataba kama sababu ya kusitisha mkataba.

"Ulikuwa mkataba wa miaka 10 ukavunjwa ndani ya miaka mitatu. Aliponipa notisi ya siku 30 nilijitahidi mimi kutafuta suluhu ilishindikana. Notisi ilieleza kwamba kuna kipengele katika mkataba kilichovunjwa cha kutowasilisha kazi ambayo ilikuwa ni albamu," Anjella alieleza.

Aliongeza, "Kipindi hicho mimi nilikuwa naumwa na nilitoa taarifa lakini wenyewe walikuwa wanahitaji kazi yao. Hapo ni mimi nilifeli. Tulijitahidi kutafuta suluhu hadi kufikia BASATA lakini ikashindikana."

Kuelekea mwishoni mwa mwaka jana, Anjella alidaiwa kutofautiana na bosi huyo wake wa zamani katika suala lisilojulikana hadi kupelekea kusitishwa kwa mkataba wake na lebo ya Konde Music Worldwide. 

Harmonize alithibitisha kuwa msanii huyo wake wa zamani  angeondoka Kondegang mnamo mwezi Novemba mwaka jana na akatoa wito kwa yeyote ambaye alikuwa tayari kuendelea kutoka alikoachia kumsajili.

“Nilikutana na Anjella akiwa amejikatia tamaa akiwa na ndoto kichwani. Sikujiangalia nina kiasi gani, nilijiamini kwa kuwa wapo watu wanaonisapoti bila kuwalipa senti tano basi watasapoti kipaji cha dada Anjella. Nilichoangalia ni ndoto na hasa za mtoto wa kike.

Nimejitahidi kadiri ya uwezo wangu, najua kuna wenye uwezo mkubwa kunizidi, ukizingatia nimeanza juzi. Kama kunaye anayeweza kumwendelezea kipaji chake ni faraja kwangu, asisite kujitokeza," alisema.

Aidha aliwataka watu kupunguza siasa kuhusu sababu ya kuondoka kwa Anjella na kuweka wazi kuwa hakudai hela zozote kutoka kwake.

Angella alithibitisha kuondoka kwake Kondegang mwanzoni mwa mwaka huu huku akiiga familia hiyo yake ya zamani.