Siku chache baada ya msanii Stevo Simole Boy kulia njaa kutokana na mzozo kati yake na uongozi wa kazi zake za Sanaa, wasanii mbali mbali wa humu nchini wamejitokeza kumpa msaada mwenzao.
Msanii huyo siku moja iliyopita alikutana na mchekeshaji Mulamwah katika ukumbi wa Sanaa wa KNT jijini Nairobi na Mulamwah alimkwamua kwa kiasi cha shilingi elfu 5 ambapo Stevo alijawa na furaha.
Stevo akizungumza na Mulamwah, alipata kueleza kwa upana shida imekuwa wapi mpaka kulazimika kurudi tena sakafuni licha ya jina lake kuwa kubwa kwenye Sanaa ya muziki wa humu nchini.
Kwa mujibu wa nyota huyo wa Mihadarati, uongozi wake, MIB ndio ambao umemuangusha vibaya, ambapo aliteta kwamba kutoka mwezi Januari mwaka huu hajawahi pata nafasi ya kutumbuiza kwenye tamasha lolote, jambo ambalo alisema ni menejimenti yake imezembea kazini.
Pia alisema kuwa uongozi huo umekuwa ukipakia kazi za wasanii wengine kwenye Instagram badala ya kumsukuma yeye, na kutangaza kwamba sasa kwenda mbele hataki tena kujihusisha na lebo yoyote bali atakuwa anajifanyia kazi mwenyewe.
“Menejimenti haifanyi kazi nzuri, ukiangaia Instagram, badala aposti msanii wake, anaposti wasanii wengine. Hanisukumi mimi. Kuna kazi zingine bado hazijatoka lakini hazinisaidii kabisa. Ukiangalia kuanzia Januari, sijapiga shoo. Unajua sihitaji pesa nyingi elfu elfu 100 hapana, ukipata 50k, 30k ama 20k, si hiyo ni sawa, inajaza kibaba. Sasa nimeamua kuwa meneja kivyangu, pamoja na marafiki zangu ambao watanisaidia,” Stevo alimwambia Mulamwah.
Stevo walikuwa na mrembo wake Grace Atieno na baada ya Mulamwah kumpokeza elfu 5, alimpa pia mrembo huyo elfu 3 za kuwasukuma katika siku hiyo wakiendela kunyoosha mambo yao.
Mulamwah alimshauri Stevo kuachana kabisa mambo na menejimenti na badala yake kufanya kazi yake kivyake, huku pia akimtaka kama uongozi umeshikilia akaunti za mitandaoni asihofu kuanza upya.
Stevo alisema kuwa usanii ni mzuri lakini pia akasema kuwa anaweza kufanya kazi kwenye kituo chochote cha redio.
“Usanii ni mzuri pia lakini pia ningependelea kama kuna kituo cha redio pale kinataka Stevo Simple Boy akuje na kuwa mtangazaji naweza. Mimi nimeamua kuwa meneja kivyangu nikiwa na mke wangu na marafiki zangu wachache,” msanii huyo alisema.