Mwanatiktok mwenye utata Brian Chira hatimaye amekutana na mchekeshaji Oga Obinna miezi kadhaa baada ya video yake kusambaa akilia huku akimwita Obinna.
Katika mahojiano na mchekeshaji huyo kwenye chaneli yake ya YouTube, Obinna alimuuliza ni kwa nini alikuwa analia na kujigaragaza akiliita jina lake na Chira akaweka waziwazi kwamba alikuwa amepagawa na bado anapagawa na yeye.
“Kusema ukweli Obinna unakaa vizuri, nafikiri nilikuwa nimepagawa na wewe, na bado nahisi nimepagawa na wewe, kwa muktadha wa maudhi. Na ikiwa kuna mtu ambaye nilikuwa nataka anikuze na kunishika mkono katika sekta ya radio kwa sababu hiyo ndio kazi nataka, basi wewe ndio mtu wa kwanza ambaye ningependa,” Chira alisema.
Hata hivyo, baada ya kutamka kwamba anapagawa na Obinna, mchekeshaji huyo alimkatisha kwa haraka na kumtaka kukoma kusema hivyo la sivyo mahojiano hayo yatamatishwe mara moja.
Hapo ndipo Chira alieleza wazi kwamba si kupagawa ambako wengi wanaweza kufikiria bali ni kupagawa kwa muktadha wa ukuzaji maudhui.
Itakumbukwa hii si mara ya kwanza kwa tiktoker huyo kuibua madai tatanishi kuhusu suala la LGBTQ, kwani miezi kadhaa nyuma alifanya video kwenye TikTok yake akikiri mapenzi yake kwa mwanablogu Andrew Kibe ambapo alisema kuwa anapagawa na ndevu zake.
Chira alisema kuwa kipindi hicho ndio mara ya kwanza alikuwa amefanya video akielezea ulimwengu kwamba alikuwa anaugua virusi vya UKIMWI na alikuwa anapitia msongo wa mawazo kwa kufikiria jinsi watu watakuwa wanamchukulia na kumuona.