"Heshimu uzee, ni kesho yako!" Mkewe Guardian Angel, Esther Musila awajibu wakosoaji

“Heshimu uzee. Ni kesho yako ooo! Nina umri wa miaka 18 hadi nife," Bi Musila alibainisha.

Muhtasari

•Esther amesema bado ana miaka 12 kabla ya kufikia umri wa kustaafu katika UN ila akadokeza hataki kusubiri ila badala yake anapanga kustaafu mapema.

•Pia alifichua kuwa kazi yake ya kwanza ilikuwa katika Ikulu na aliipata baada ya kutuma maombi zaidi ya mia moja.

Mke wa mwimbaji wa nyimbo za injili Guardian Angel, Esther Musila amewajibu wakosoaji wake ambao wamekuwa wakimkosoa kuhusu mpango wake wa kustaafu.

Katika taarifa yake siku ya Ijumaa, mhasibu huyo mwenye umri wa miaka 53 alibainisha kuwa watu kadhaa wamekuwa na maswali chungu nzima baada ya kufanya mahojiano na kufichua kuwa ana mpango wa kustaafu katika shirika la Umoja wa Mataifa (UN) katika miaka mitano ijayo baada ya kufanya kazi huko kwa zaidi ya miongo miwili.

Esther ameweka wazi kwamba bado ana miaka 12 kabla ya kufikia umri wa kustaafu katika Umoja wa Mataifa lakini akadokeza kuwa hataki kusubiri ila badala yake anapanga kustaafu mapema.

”Kwa wale mnaouliza baada ya kuona mahojiano yangu, umri wa kustaafu katika UN ni miaka 65! Bado nina miaka 12 zaidi ya kufanya kazi nikitaka, lakini nina chaguo la kuondoka mapema..,” Esther alisema kupitia mtandao wa Instagram.

Aliongeza, “Heshimu uzee. Ni kesho yako ooo! Nina umri wa miaka 18 hadi nife.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na Standard Entertainment & Lifestyle, mke huyo wa mwanamuziki wa Injili Guardian Angel alifichua kuwa anataka kustaafu hivi karibuni ili aanze kufurahia pesa zake kabla hajazeeka sana.

"UN imekuwa kazi yangu bora. Miaka 21 si muda mfupi, ni muda mrefu. Hivi karibuni ninatazamia kustaafu, labda katika miaka mitano ijayo. Nitakuwa nikistaafu, nataka kufurahia pesa zangu nikiwa bado mdogo,” Bi Omwaka alisema.

Mama huyo wa watoto watatu alizungumza kuhusu jinsi alivyopata kazi yake ya kwanza katika Umoja wa Mataifa takriban miongo miwili iliyopita.

Alifichua kwamba alikuwa ameajiriwa kwanza kujaza nafasi ya mwanamke ambaye alikuwa amechukua likizo ya uzazi.

"Kila kitu nilichofanya, nilijifunza kazini, sio kama nilikuwa nimeisomea. Baada ya wakati fulani nilihama kutoka idara ya Ufuatiliaji na Tathmini. Kisha baada ya miezi michache, yule mwanamke niliyekuwa nimechukua mahali pake akajiuzulu. Nini kilitokea, Esther alipata kazi. Baada ya hapo nilihamia idara nyingine ambapo nilikuwa nikishughulika na vijana. Kulikuwa na hazina ya vijana, nilishirikiana sana na vijana. Huo ulikuwa wakati mzuri katika kazi yangu,” alisema Esther.

Esther alifichua kuwa amefanya kazi katika idara nyingi za UN kabla ya kufika katika idara ya Usimamizi wa Miradi ambako anafanya kazi kwa sasa.

"Nimefanikiwa kupanda ngazi kupitia bidii na mafunzo kazini na kuweza kutaka kufanya mambo mapya," alisema.

Pia alifichua kuwa kazi yake ya kwanza ilikuwa katika Ikulu na aliipata baada ya kutuma maombi zaidi ya mia moja.

Esther Musila alisoma Ukatibu katika Chuo cha Kianda baada ya kumaliza kidato cha nne.