Professor Jay, mkewe washerehekea maisha na afya huku wakiadhimisha kumbukumbu ya harusi

Mwaka jana Professor Jay alilazwa katika ICU kwa takriban siku 127 baada ya kushambuliwa na ugonjwa hatari.

Muhtasari

•Wanandoa hao wamesherehekea safari yao ya ndoa na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwaweka pamoja kwa miaka ambayo wamekuwa pamoja.

•Asante sana Mke wangu kipenzi kwa kuvumilia mapito yote tuliyotupitia pamoja sina la kusema zaidi ya NAKUPENDA SANA," Jay alimwambia mkewe.

Professor Jay na mkewe Grace Mgonjo
Image: INSTAGRAM

Siku ya Jumamosi, Julai 8, rapa mkongwe wa Tanzania Joseph Haule almaarufu Professor Jay na mke wake Grace Mgonjo walisherehekea kumbukumbu ya ndoa yao.

Wanandoa hao walitumia kurasa zao za mitandao  ya kijamii kusherehekea safari yao ya ndoa na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwaweka pamoja kwa miaka ambayo wamekuwa pamoja.

Professor Jay ambaye takriban mwaka mmoja uliopita aliruhusiwa kutoka hospitalini baada ya kulazwa katika ICU kwa zaidi ya siku 100 alitumia fursa hiyo kumshukuru mke wake kwa kumsaidia na kusimama naye katika yote waliyopitia.

“Asante sana Mwenyezi Mungu kwa kutupa zawadi hii ya Uhai na kuwa pamoja nasi mpaka Leo tunapoadhimisha siku yetu ya kufunga ndoa yetu takatifu, Asante sana Mke wangu kipenzi @mke_wa_profjize kwa kuvumilia mapito yote tuliyotupitia pamoja sina la kusema zaidi ya NAKUPENDA SANA,” Professor Jay alisema kwenye mtandao wa Instagram.

Aliambatanisha ujumbe huo na picha yake na mke huyo wake mrembo wakiwa wamesimama nje ya nyumba yao.

“Tuendelee kumtumaini Mwenyezi Mungu aliye hai siku zote za maisha yetu ,Naamini yeye pekee ndiye anayeweza kutupigania na kutuvusha salama siku zote za maisha yetu, Happy anniversary to us my beautiful wife,” aliandika.

Bi Haule pia alituma shukrani zake kwa Mungu kwa kuwajalia uhai na afya njema ili kusherehekea siku yao hiyo maalum.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, alijitakia yeye na mwimbaji huyo mkongwe kheri njema ya siku ya kuadhimisha ndoa yao.

“Mungu Asante Kwa kutuwezesha kuwa hai na kuona tena siku ya leo tukiwa wazima na wenye afya njema @professorjaytz. Sina la zaidi ya kukurudishia sifa na utukufu eeeh Mungu,” Bi Grace aliandika.

Mapema mwezi Mei, Profesa Jay alivunja kimya kwenye mitandao ya kijamii, miezi kadhaa baada ya kupambana na ugonjwa hatari ambao ulitishia maisha yake.

Katika chapisho lake la kwanza baada ya takriban mwaka mmoja na miezi minne, Jay ambaye pia ni mbunge wa zamani wa eneo la Mikumi nchini Tanzania alitoa taarifa kuhusu maendeleo ya afya yake baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini ambapo alibainisha kuwa sasa yupo imara na anaendelea vizuri.

Jay alisema kwamba alikuwa katika hali mbaya sana akibainisha kwamba Mungu alimuokoa kutokana na hali hiyo.

"Kwanza namshukuru sana MUNGU aliye hai kwa uponyaji na kunipa nafasi nyingine ya kuendelea kuwa hai, Hali yangu ilikuwa mbaya isioelezeka, Asante sana Mungu baba, nitakutukuza na kukusifu siku zote za maisha yangu," alisema katika taarifa ambayo alichapisha kwenye mtandao wa Instagram.

Rapa huyo aliendelea kutoa shukrani za dhati kwa wote ambao walisimama naye katika kipindi cha maumivu yake wakiwemo rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ambaye aligharamia matibabu yake, kiongozi wa chama cha CHADEMA Freeman Mbowe miongoni mwa viongozi wengine.

"Namshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Dr. Samia Hassan Suluhu na Serikali yake kwa kunigharamia matibabu yangu yote ya Muhimbili na Nje ya Nchi ,Asante sana Mama pamoja na serikali yako yote kwani viongozi wako wa chama na serikali walikuwa wanapishana kila siku kuja kuniona na kunifariji."

Namshukuru sana Mwenyekiti wa chama changu cha CHADEMA Kamanda @freemanmbowe ,Wanachama na viongozi wote waandamizi wa chama kwa jitihada zao za kuhakikisha napata matibabu bora zaidi kwa kushirikiana na serikali." alisema.

Jay pia aliwashukuru wahudumu wa afya ambao walifanya juu chini kuhakikisha kuwa afya yake imerejea hasa alipokuwa ICU siku 127.