Muigizaji na mwanamitindo mkongwe wa Bongo, Wema Sepetu amesisitiza kuwa yeye si mjamzito kama ilivyodokezwa awali kwenye video iliyosambaa mtandaoni.
Akizungumza na wanahabari mwishoni mwa wiki, Miss Tanzania huyo wa zamani alibainisha kuwa video iliyohaririwa ikimuonyesha akiwa mjamzito ambayo ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii wiki iliyopita ilimfanya ahisi kilio.
“Ilinifanya nipate hisia sana. Nilimtumia Chibaba (video) nikamwambia hichi kitu kimenifanya mpaka nikalia. Akaniambia nisijali, ni sawa, ni kitu ambacho ni watu wanakutakia na wanakuombea. Kama wanakuombea basi ni kitu kiko positive. Tukichukulie kama positive,” Wema Sepetu alisema.
Mpenzi huyo wa zamani wa bosi wa WCB Diamond Platnumz alifichua kuwa kufuatia video hiyo alipokea maswali mengi na jumbe za pongezi kutoka kwa watu walioamini kuwa ni mjamzito baada ya kuiona video hiyo.
Alisema jumbe nyingi alizopokea zilimsukuma kufafanua mambo na kutupilia mbali uvumi huo wa ujauzito.
“Kwangu mimi watu walikuwa wananiuliza sana maswali. Kwa sababu sio watu wengi wanakuwa wananiona mara kwa mara, wengine wakiona video wanaona kweli mimi ni mjamzito. Maswali yalikuwa ni mengi, hongera pia zilikuwa nyingi,” alisema.
Aliongeza, “Ilibidi nipost kitu ili kuwaambia mashabiki wangu na watu ambao wanapenda kwamba sio kile ambacho walikuwa wakifikiria. Lakini kwa kweli nitatamani sana siku moja.”
Katika mahojiano hayo, muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 35 pia alifunguka kuhusu tatizo la uzazi ambalo limemfanya hajafanikiwa kuwa na mtoto kufikia sasa.
Alidokeza kwamba amewahi kupata ujauzito mara kadhaa katika siku za nyuma ila hakuweza kufikia hatua ya kujifungua.
"Niko na shida ya kizazi. Huwanga nikipata mimba mara nyingi sifiki miezi miwili mitatu mimba inaharibika. Ilitokea, lakini bahati mbaya," alisema.
Aiidha, alisema itakuwa ndoto yake iliyotimia kupata mtoto na mume wake Whozu.
"Nimekuwa nikitamani sana mtoto. Lakini chochote kitakachotokea kwanza, iwe mtoto kwanza ama harusi ni sawa," alisema.
Wema na mwimbaji Whozu walifichua mahusiano yao mwaka jana baada ya kuchumbiana kwa muda.