Akothee awasuta binti zake kwa kumzuia kucheza muziki aupendao kwenye gari lake

“Wajinga hawa wasingeniruhusu kucheza muziki wangu wa sauti ya juu wa Kijaluo kwenye gari langu!" Akothee alilalamika.

Muhtasari

•Akothee aliwakosoa binti zake kwa kumzuia kucheza muziki aupendao wa Kiluo kwenye gari lake katika siku za nyuma.

•Akothee amewashauri wazazi wengine wasiache kufurahia maisha yao wanavyotaka kwa sababu tu ya watoto wao.  

Akothee na mabinti zake
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na mjasiriamali Esther Akoth almaarufu Akothee ameshangazwa na mabadiliko ya ghafla katika ladha ya muziki ya binti zake.

Katika taarifa yake siku ya Jumapili, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 aliwakosoa binti zake kwa kumzuia kucheza muziki aupendao wa Kiluo kwenye gari lake katika siku za nyuma.

Akothee alifichua kwamba binti zake  wangechagua kutosafiri naye kwa gari moja ili tu wasiende wakisikiliza muziki anaopendelea kusikiliza.

“Wajinga hawa wasingeniruhusu kucheza muziki wangu wa sauti ya juu wa Kijaluo kwenye gari langu, wangependelea hata kwenda na dereva kwenye gari tofauti kwa sababu ya muziki wangu wa kuchosha hasa Juma Limpopo International na leo wamenunua magari zao na ona sasa ni nani nyar masayi ,” Akothee alisema.

Aliambatanisha taarifa hiyo na video ya binti yake wa kwanza Vesha Okello na rafikiye wakifurahia wimbo wa Onyi Papa Jey Nyar Maasai ndani ya gari. Wawili hao walionekana kuwa na furaha tele huku wakicheza na kuimba wimbo huo pamoja na mwimbaji.

Katika maelezo ya video hiyo, Vesha alidokeza kwamba sasa anapenda kusafiri kwa gari huku akisikiliza muziki wa Kijaluo wa sauti ya juu.

"Kama safari ya gari haiko hivi sitaki," Vesha alisema.

Katika taarifa yake, Akothee alilalamika kwamba alipokuwa akisafiri na binti zake katika siku za nyuma walikuwa wakilalamika kuwa kila  wakati alikuwa anaweka muziki wa Kijaluo kwa sauti kubwa na kuimba pamoja na mwimbaji.

Hata hivyo, amedokeza anafurahi kwamba hakubadilisha ladhaa  yake ya muziki kwa sababu yao kwa vile sasa wanaonekana kubadilika pia.

"Uzazi ni utapeli. Namshukuru Mungu sikuwahi kuwasikiliza, wakati huu ningekuwa na hasira sana," alisema.

Kutokana na hilo, amewashauri wazazi wengine wasiache kufurahia maisha yao wanavyotaka kwa sababu tu ya watoto wao.