"Kama uliroga mwanangu nisamehe"Justina Syokau azungumzia ugonjwa wa mwanawe kwa hisia

Justina alisema madaktari bado hawajafaulu kujua ni nini hasa mvulana huyo wa miaka 10 amekuwa akiugua.

Muhtasari

•Justina alifichua kuwa mwanawe amekuwa akiugua mara kwa mara tangu mwezi Desemba mwaka jana.

•Justina ameomba msamaha kwa Wakenya huku akidokeza ugonjwa wa mwanawe unaweza kuwa ulitokana na nguvu za giza.

Image: INSTAGRAM// JUSTINA SYOKAU

Mwimbaji wa nyimbo za Injili mwenye utata Justina Syokau almaarufu ‘twendi twendi’ amefunguka kuhusu ugonjwa wa mwanawe ambao umefanya miezi kadhaa iliyopita kuwa kipindi kigumu kwake.

Akizungumza katika mahojiano na Mungai Eve Media, Justina alifichua kuwa mwanawe amekuwa akiugua mara kwa mara tangu mwezi Desemba mwaka jana.

Alisema ugonjwa usiojulikana ambao mwanawe amekuwa akiugua ulianza baada ya kwenda kuwatembelea familia yao kijijini.

“Mambo yamekuwa magumu kutoka mwaka wa 2023 uanze.  Desemba nilikuwa nimempeleka mtoto wangu nyumbani kwa sababu alikuwa anataka kusalimiana nyumbani, hajawahi kwenda tena. Niliamua kumpatia nafasi ya kwenda nyumbani kwa siku 10, nadhani alikaa wiki tatu. Na aliporudi Nairobi hajawahi kuwa sawa. Amekuwa akiugua mara kwa mara,” Justina alisimulia.

Aliongeza, "Katika muhula wa kwanza, hakuweza kuwa shuleni kwa sababu alikuwa mgonjwa sana. Tumetembelea hospitali nyingi na mwanangu na imekuwa ngumu sana. Hata saa hii, muhula huu amesoma bado akiwa mgonjwa. Namshukuru Mungu ana nguvu.”

Mwimbaji huyo wa nyimbo za injili alibainisha kuwa mwanawe amekuwa na afya njema kwa miaka mingi na hakuwa akiugua magonjwa yoyote kabla ya mwishoni mwa mwaka jana.

Alifichua kuwa madaktari bado hawajafaulu kujua ni nini hasa mvulana huyo wa miaka 10 amekuwa akiugua.

“Ukimpeleka hosi unaambiwa mtoto ako sawa. Kuna wakati tukienda hospital unapata ugonjwa hupatikani. Kuna wakati tunaambiwa digestion yake ndiyo iko na shida ama koloni yake ndiyo iko na shida,” alisema.

Alifunguka kuhusu jinsi ugonjwa wa mwanawe umeathiri taaluma yake ya muziki na jinsi amepoteza pesa nyingi wakati akijaribu kumtafutia matibabu.

Sasa ameomba msamaha kwa Wakenya huku akidokeza kwamba ugonjwa wa mwanawe unaweza kuwa ulitokana na nguvu za giza zilizotumwa na mtu ambaye huenda aligongana naye hapo awali au mwenye chuki dhidi yake.

“Naomba kama kuna mtu nimekosea, naomba mnisamehe. Kama kuna kitu nishawahi kufanyia mtu kikakukwaza na ndicho kimefanya mimi nifike mahali nimefika, naomba mnisamehe. Kama kuna mtu aliweza kunifanyia kitu mtoto wangu, labda uliroga mtoto wangu. Kama kuna mtu nilikosea mahali na akafanya kitu kikaathiri mtoto wangu. Heri kingeniathiri mimi kuliko kuathiri mtoto. Nahisi nafaa kusema pole kwa watu,” alisema mwimbaji huyo.

Justina ni mama wa mtoto mmoja ambaye anagonga umri wa miaka 10 mwezi Agosti. Hata hivyo, alitengana na mzazi mwenzake maika kadhaa iliyopita na amekuwa akiishi na mvulana huyo pekee.