Muigizaji Sandra Dacha amesimulia maisha yake ya utotoni na kusema kwamba akiwa shuleni kutoka la kwanza hadi kidato cha nne, hakuwahi tongozwa na mvulana yeyote wa shuleni.
Dacha alisema kwamba wengi wa watu ambao walikuwa wanamtongoza akiwa shuleni ni watu wakubwa kiumri kumliko na ambao hawakuwa wanafunzi.
Muigizaji huyo alimwambia Oga Obinna hadithi yake kwamba hilo lilimtokea kwa sababu alikuwa mnene na kila mvulana wa rikka lake alikuwa anamuogopa.
Dacha alisema kuwa ukubwa na unene alio nao kwa sasa hivi na ambao ameukumbatia kwa kujipa jina la kimajazi ‘Biggest Machine’ hajaupata ukubwani bali alizaliwa nao, akiwa na uzani mkubwa sana siku ya kwanza duniani.
“Unaweza amini wakati nilikuwa shuleni sikuwahi tongozwa na mvulana hata mmoja, hakuna mvulana yeyote wa shule za upili aliyenitongoza, lakini nilitongozwa na Wababa,” alifunguka.
Sababu ya vijana wa rika lake kumuogopa na wanaume watu wazima kumuona kama mtu mzima wa kutongozwa, Dacha alisema ni unene wake ulimponza na kumweka kwenye jaribu hilo.
“Unajua mimi sijawahi kuwa mwembamba katika maisha yangu yote. Mimi nilizaliwa kama niko na uzani wa kilo 6 tayari. Sasa hivi nina uzani wa kilo 130. Nikiwa shule, watu walikuwa wananiita matron, nilikuwa mkubwa kuliko vile niko sasa hivi,” Dacha alielezea.