“Kuja kwako kumenifunza vingi!” Hamisa Mobetto amsherehekea mwanawe huku Diamond akimpuuza

Hamisa Mobetto alibainisha kuwa kuzaliwa kwake kulileta mabadiliko mengi katika maisha yake.

Muhtasari

•Mtoto wa pili wa mwanamitindo mashuhuri wa Tanzania Hamisa Mobetto, Dylan Abdul Naseeb anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

•Swali la ni nani baba halisi wa mtoto wa pili wa mwanamitindo Hamisa Mobetto limebaki kuwa kitendawili tu.

amemsherehekea mwanawe huku Diamond akimpuuza.
Hamisa Mobetto amemsherehekea mwanawe huku Diamond akimpuuza.
Image: INSTAGRAM//

Hivi leo, Agosti 8, mtoto wa pili wa mwanamitindo wa Tanzania Hamisa Mobetto, Dylan Abdul Naseeb anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Mama huyo wa watoto wawili alizamia kwenye mitandao ya kijamii kumsherehekea Dylan kwa ujumbe mzuri anapotimiza miaka sita.

Katika ujumbe wake kwa mwanawe huyo wa pekee, Hamisa alibainisha kuwa kuzaliwa kwake kulileta mabadiliko mengi katika maisha yake.

“Kuja Kwako kumenifunza vingi na kumenibadilisha vingi pia, Ahsante Kwa Kuendelea Kunifanya Mama Wa Kipekee Kwako, Kila Nikuonapo Ukiwa Na Tabasamu Hunifanya Nijione Mwenye Bahati Kuwa Nawe,” Hamisa aliandika.

Mpenzi huyo wa zamani wa bosi wa WCB Diamond Platnumz alidokeza kuwa Dylan hakuleta mabadiliko katika maisha yake pekee bali pia alileta athari nzuri katika maisha ya binti yake, Fantasy Majizzo.

“Umenipa Amani Pale Napokuwa Na Wasiwasi, Umenipa Furaha Pale Napokuwa Na Huzuni, Zaidi Ya Yote Umenifanya Bora Si Kwako Tu Bali Hata Kwa Dada Yako,” Hamisa Mobetto alimwandika mwanawe.

Aliongeza, “Endelea kukua kwenye Njia iliyonyooka, Ninakuahidi Malezi Bora Na Kwa Baraka Za Mungu Utakuja Kuwa Mtu Ambaye Dunia Itajivunia Siku Moja."

Aidha, Hamisa alimshukuru Dylan kwa kuwa mtoto mzuri kwake na kumtakia kila la heri anaposherehekea siku yake maalum.

Licha ya mwanamitindo huyo wa Tanzania kumsherehekea mwanawe kwa ujumbe mzuri, mwanamuziki Diamond Platnumz ambaye wengi wanaamini kuwa ndiye baba wa mvulana huyo mdogo alikuwa bado hajamwandikia ujumbe wowote kufikia wakati wa kuchapishwa kwa makala haya.

Hili si la kushangaza sana kwani staa huyo wa bongo pia hakumsherehekea Dylan mnamo siku yake ya kuzaliwa mwaka jana.

Swali la ni nani baba halisi wa mtoto wa pili wa mwanamitindo Hamisa Mobetto limebaki kuwa kitendawili tu huku Diamond mara nyingi akionyesha dalili za wazi kuwa hamkubali au kumtambua mvulana huyo kuwa mwanawe.

Siku chache zilizopita, rapa wa bongo Bill Nass alijitenga mbali na madai yanayomhusisha na mvulana huyo wa miaka sita.

Kwa muda mrefu, watu wamekuwa wakihusisha mtoto wa pili wa mwanamitindo huyo na Bill Nass na hata kuibua madai kuwa wanafanana sana. Bill Nass hata hivyo amedokeza kuwa tetesi za yeye kuwa baba wa mtoto huyo ni propaganda tu na kusema kuwa tayari Hamisa alikuwa na watoto wake wawili wakati walipofahamiana.

“Ni propaganda za watu. Sijui nia au dhumuni ya hiyo habari ilianzia wapi lakini mimi mtoto hanihusu kwa namna moja au nyingine. Wakati ambao tulifahamiana, tayari alikuwa na watoto wake wawili. Kwa mara ya kwanza namuona alikuwa na watoto. Kutokea hapo sijawahi kuwa na issue yoyote,” alisema kwenye mahojiano na Wasafi Media.