Muigizaji mkongwe wa filamu bongo Fridah Kajala Masanja ametania uvivu wa binti yake Paula Paul kabla ya kuingia kwenye ndoa.
Katika chapisho la Instagram siku ya Ijumaa, mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize alimuomba Mungu amsaidie binti yake aweze kuwa mvumilivu kwa wakwe zake.
Kajala alichapisha meme kuhusu mwanamke kuwa mvivu na kuishia kuoelewa katika familia ambapo wakwe wanapenda kutumana tumana.
“Ulivyo mvivu na wakwe wanavyopenda kutuma tuma utavumilia kweli?’" meme hiyo ilisomeka.
Muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 40 alimtaja binti yake Paula na kudokeza kwamba Mungu alihitajika sana kuingilia kati katika kesi yake.
“@therealpaulahkajala Mungu akusimamie,” Kajala aliandika.
Paula alichapisha tena chapisho la mama yake kwenye akaunti yake rasmi na akacheka tu kejeli ya muigizaji huyo ya kimakusudi.
Haya yanajiri wakati Paula amezama kwenye dimbwi zito la mahaba na staa wa bongo Omary Mwanga almaarufu Marioo ambaye amekuwa akichumbiana naye kwa muda wa miezi kadhaa iliyopita. Penzi la wawili hao limeonekana kuendelea kunoga kadiri siku zinavyosonga na wawili hao hawaona haya kulionesha hadharani.
Kajala ameonekana waziwazi kukubali mahusiano ya bintiye na Marioo na hata mara nyingi ameonekana akiyapigia debe.
Mapema wiki hii, Kajala alikiri kwamba tayari Marioo ameshapeleka barua ya posa kwa familia yake kwa ajili ya kupata ndio ya kumchumbia Paula.
Kajala hata hivyo, alionekana kutoa onyo kwa msanii huyo na kumuambia kwamba ikija kutokea wamekosana na wakaachana, hafai kuanza kumchamba bintiye kama ambavyo Harmonize amekuwa akimchamba yeye na Paula mitandaoni.
Muigizaji huyo alivuka mipaka hata zaidi na kumtishia Marioo kuwa iwapo atafanya hivyo, basi hatokuwa na budi bali kumroga tu.
“Hongera mwanangu, bonge moja la video, kuhusu barua ya uchumba tumeipokea kwa mikono miwili subiria majibu na karibu familia ya Masanja family. (ila mwakani usije ukatuchamba na wewe nitakuroga)” Kajala alisema japo kwa utani wakati akiupigia debe wimbo mpya wa mkwewe kwenye Instagram yake.
Wapenzi hao wamekuwa wakichumbiana kwa miezi kadhaa iliyopita tangu walipoweka wazi mahusiano yao mwezi Aprili. Marioo anaonekana kuwa na uhusiano mzuri, si tu na Paula bali pia na mama mkwe wake Kajala Masanja.
Paula alitangaza mahusiano yake na Marioo Aprili, muda mfupi baada ya aliyekuwa mpenziwe, Rayvanny kurudiana na Fahyma.