Zari Hassan afichua vitu 8 maalum anazoleta kwenye ndoa

"Mimi ni aina ya mwanamke anayeleta mengi kwenye meza," Zari alijigamba.

Muhtasari

•Katika chapisho la siku ya Jumanne, mama huyo wa watoto watano alitaja mambo manane maalum ambayo huwa analeta katika ndoa.

•Mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz kwa sasa yuko kwa ndoa na mfanyibiashara wa Uganda Shakib Cham Lutaaya.

Shakib na Zari
Image: INSTAGRAM// SHAKIB

Mwanasosholaiti na mfanyibiashara maarufu wa Uganda Zari Hassan amejigamba kuwa aina ya mwanamke ambaye ana mengi ya kutoa kama mke.

Katika chapisho la siku ya Jumanne, mama huyo wa watoto watano alitaja mambo manane maalum ambayo huwa analeta katika ndoa.

Zari alishiriki video nzuri iliyomuonyesha akisimama juu ya jengo la ghorofa na kuorodhesha baadhi ya mambo anayoleta kama mke.

"Mimi ni aina ya mwanamke anayeleta mengi kwenye meza. Upendo, akili, hekima, kusudi, hadhi, nia ya makuu, thamani na msukumo #bosslady,” Zari alisema.

Mpenzi huyo wa zamani wa staa wa bongo Diamond Platnumz kwa sasa yuko kwa ndoa na mfanyibiashara wa Uganda Shakib Cham Lutaaya.

Wawili hao walifunga ndoa Aprili mwaka huu baada ya kuwa wamechumbiana kwa takriban mwaka mmoja. Walivishana pete katika hafla ya faraghani ambayo ilihudhuriwa na idadi ndogo ya watu wakiwemo wanafamilia na marafiki.

Katika picha na video hafla hiyo iliyofanyika chumbani ambazo zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii, wapenzi hao walionekana wamevalia Kiislamu kabisa huku wote wakiwa wameketi kwenye mkeka uliotandikwa sakafuni.

Wajati wa hafla hiyo, Shakib alionekana akiinama kwa goti moja na kumvisha Zari pete ya ndoa kwa furaha kabla ya wawili hao kupigana mabusu huku watu wachache waliohudhuria hafla hiyo wakiwasherehekea kwa makofi.

Takroban miezi minne iliyopita, Zari aliokeza kuwa alichumbiana na Shakib kabla ya kujitosa kwenye ndoa na Diamond Platnumz.

Katika mahojiano, mama huyo wa watoto watano alikiri kuwa amemfahamu mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 31 kwa miaka kadhaa sasa. 

Alikiri kwamba yeye na Shakib walichumbiana miaka kadhaa nyuma kabla ya kutengana na kurudiana tena mwaka jana.

"Nilichumbiana na Shakib huko nyuma kisha tukaenda njia tofauti. Sijui tulipatana vipi tena," Zari alisema.

Mzazi mwenza huyo wa Diamond Platnumz alisema haikuwa ngumu kuungana tena na Shakib na kufunga naye ndoa mwezi uliopita kwani waliwahi kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi katika siku za nyuma .

"Mwaka moja baada ya kurudiana alisema nitakufanya mke wangu. Ni hayo tu. Hatukuzungumza kwa muda kisha ghafla mwaka mmoja baada ya kurudiana tukafunga ndoa. Ikiwa sio Mungu, tutaiitaje hiyo?," alihoji.

Zari alirudiana na Shakib mapema mwaka jana baada ya kukatiza mahusiano na mfanyibiashara wa Uganda GK Choppa. Waliweka mahusiano yao siri hadi katikati mwa mwaka jana ambapo walifichua wanachumbiana.