Shabiki wa Man U alazwa baada ya kula mayai 15 kwa kupoteza dhidi ya Arsenal

Kapkeno alikuwa ameahidi kula trei ya mayai ya kuchemshwa iwapo timu ya Man United ingeshindwa.

Muhtasari

•Ili kulainisha chakula chake kilicho jaa protini,Kapteno alikua na chumvi pamoja na mchuzi wa nyanya pembeni. 

•Marafiki wa Kapkeno waliodhani alikuwa akiwatania, wanasikika kwenye kanda ya video wakiangua kicheko huku wakimtia moyo atimize ahadi yake.


Image: FACEBOOK// KAPKENO

Shabiki mmoja wa Manchester United kutoka mji wa Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu aliishia pabaya baada ya kupoteza dau 

Thomas Kiptanui Kemboi,anayejulikana kwa jina la majazi Kapkeno, alikua ameahidi kula trei ya mayai ya kuchemshwa iwapo timu ya Manchester United anayoishabikia ingeshindwa katika mechi dhidi ya Arsenal iliyochezwa wikendi ya Jumapili Julai 3 katika ligi kuu ya Uingereza.

Mechi hiyo ilikamilika, kwa Arsenal ikiwacharaza United mabao 3-1,matokeo ambayo yalimfanya Kapkeno kukosa budi ila kutimiza ahadi yake.

Katika kipindi cha moja kwa moja kwenye Facebook, akiwa na marafiki wake akiwemo mpiga picha wake,msanii huyo maarufu kwa wimbo wake wa 'Wachawi' alivua gamba lake na kuanza kipindi cha kula mayai moja baada ya jingine.

Ili kulainisha chakula chake kilicho jaa protini,Kapteno alikua na chumvi pamoja na mchuzi wa nyanya pembeni. Aidha alichukua mapumziko ya mara kwa mara ili  kunywa maji asije akanyongwa na  mayai.

Kapkeno aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook;

"Kutokana na kupoteza kwa Manchester United Kwa Arsenal, mimi kama Kapkeno ninatimiza ahadi yangu ya kula trei moja ya mayai kwa mashabiki wangu,

"Baada ya kumeza jumla ya mayai 15, alianguka ghafla.

Marafiki wa Kapkeno waliodhani alikuwa akiwatania, wanasikika kwenye kanda ya video wakiangua kicheko huku wakimtia moyo atimize ahadi yake.

Victor Kimutai, ambaye ni mpiga picha wake Kapkeno alisema;

"Tulidhani kuwa yote ni sehemu ya maigizo. Tulikuwa na matumaini kuwa angeweza kula mayai yote,hatukufikiri kwamba lilikuwa jambo zito na kwamba angemalizia kulazwa Hospitalini,"

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 27 alikiri kwamba kabla ya kuzimia, alikua na homa na kutokwa na jasho kupita kiasi, na tumbo lake kuanza kuvimba.

Kapkeno alieleza;

"Dakika moja nilikuwa na nguvu na tayari kukamilisha changamoto iliyokuwa mbele yangu na baadae nilikuwa Hospitalini na drip ya Iv mkononi mwangu.Niligunduliwa na tatizo la kuvimba na kudungwa viowevu vitatu vya IV na ninashukuru kwamba sasa ninaendelea vyema,

"Baadaye Kapkeno aliwaonya vijana dhidi ya kucheza kamari bila kuwajibika. Hata hivyo Kapkeno alisisitiza kwamba hilo halitomzuia kushabikia  klabu hiyo ya Manchester United.