Msanii wa Uganda Moses Ssali maarufu kama Bebe Cool ameingia kwenye vitabu vya kihistoria nchini humo baada ya kuwa msanii wa pili kununua gari lenye uwezo wa kuzuia risasi kupenyeza ndani wakati wa shambulio.
Kwa mujibu wa majarida ya burudani nchini humo, Bebe Cool alitambulisha gari hilo la kifahari aina ya Toyota Land Cruiser V8 lenye thamani ya shilingi milioni 24.2 pesa za Kenya, na kuwa msanii wa pili wa Uganda kumiliki gari hilo la kuzuia risasi.
Mnamo Februari 2022, Bobi Wine alinunua gari la kivita aina ya Toyota Land Cruiser V8, Nambari ya Usajili UBJ 667F ambayo anadai alichangiwa na wafuasi wake.
Hata hivyo, Mnamo Aprili 2022, mamlaka ya ukusanyaji ushuru Uganda, URA ilikamata gari la Bobi Wine ikihoji kuwa halikuwa na thamani. URA ilisema gari hilo lilitangazwa kuwa gari la forodha kama gari la kawaida na si lenye uwezo wa kuzuia risasi, hivyo basi, kodi hiyo ililipwa kidogo na hivyo kunahitajika ukaguzi mwingine.
Baada ya miezi miwili kutathmini gari hilo, Rais Museveni aliiagiza URA kuachilia na kumrudishia gari Bobi Wine.
Tangu wakati huo, Bobi Wine alibaki kama msanii pekee nchini Uganda kuwahi kumiliki gari la bulletproof.
Hata hivyo, mwezi uliopita maneno yalianza kuenea kwamba adui wa Bobi Wine, Bebe Cool pia alinunua gari lenye bulletproof.
Katika klipu ya video inayozunguka kwenye mitandao ya kijamii, gari la kivita la Bebe Cool linaweza kuonekana likiwa limeegeshwa katika boma lake na milango yake yote wazi alipokuwa akiwachukua wafuasi wake kuizunguka na ndani yake.