Mtumizi mmoja wa mtandao wa TkTok amewaacha wengi katika mshangao mkubwa baada ya kupakia video aliyosema alishuhudia na kuirekodi ya paka wawili wakila kutoka sahani moja panya.
Video hiyo ilipakiwa na mtu huyo kwa jina darhlinsapple93 kwenye mtandao huo na kuzua gumzo pevu mitandaoni haswa kutokana na dhana ambayo imekuwa ikijulikana tangu enzi za wahenga kwamba adui namba moja wa panya ni paka na hakuna siku viumbe hao wawili watakula kutoka kwa sinia moja.
“Hata Wanyama Wanahitaji Umoja kiasi gani Binadamu zaidi? Nimeichukua hii tu 😂” mtumizi huyo wa TikTok aliandika.
Mwanamume huyo ambaye alirekodi tukio hilo adimu alishangazwa na kitendo hicho huku akieleza mshtuko kwamba paka na panya, ambao mara nyingi huchukuliwa kuwa mwindaji na windo, wanaweza kuweka kando tofauti zao na kufurahia mlo, hivyo basi, kutengeneza tamasha la umma.
Watu wengi waliojaza sehemu ya maoni ya video hiyo walionyesha kushangazwa, huku wengi wakikubali kwamba matendo ya paka na panya kweli yana ujumbe.
Haya hapa ni baadhi ya maoni ya watu walioona video hiyo;
“Hii ina maana kubwa kwa sababu kama kuna sisi chakula kwa ajili ya wote hakuna mtu kula juu ya mtu” Abbas Quansca alisema.
“Hii inaonyesha kuwa kuna amani ndani ya nyumba hiyo na hiyo pia imewaathiri wanyama hawa” Amos aliongeza.
Wengine walisema kwamba paka hao walikuwa wanakula omena pengine hawakuona haja ya kumrukia panya huyo kwani tayari mbele yao kulikuwa na chakula cha kutosha.
Hata hivyo, wengine walitoa maoni kwamba paka wa siku hizi ni feki na huwa hawarukii panya kama ambavyo paka wa zamani walikuwa wanaeneza uadui wao dhidi ya panya.