Akothee aonyesha upendo kwa Jalang’o kwa kumchezea dansi hospitalini baada ya upasuaji (+video)

"Leo yuko chini (Jalang'o). Nitakaa naye hapa usiku huu, nicheze densi tu na kumchekesha,” Akothee alisema.

Muhtasari

•Akothee alimdensia mbunge huyo na densi ilipoisha Jalang'o aliamka kwa usaidizi wa mikongojo na  wakakumbatiana.

•Wengine waliaomtembelea Jalang’o hospitalini ni pamoja na Mbunge Babu Owino,mjasiriamali Alinur Mohamed, mwimbaji Dufla Diligon,  Ian Oparanya, Rodgers Kipembe na MCA Abass Khalif.

Image: INSTAGRAM// JALANGO

Watu mashuhuri nchini Kenya wameendelea kumtembelea mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwour almaarufu Jalang’o hospitalini na kumtakia afueni ya haraka anapoendelea kupokea matibabu.

Jalang’o amelazwa katika Hospitali ya Nairobi baada ya kupata jeraha la mguu alipokuwa akicheza mpira wa vikapu mapema wiki hii. Madaktari tayari wamemfanyia upasuaji kwenye mguu wake wa kushoto katika juhudi za kutibu jeraha lake na sasa anaendelea kupata afueni.

Siku ya Ijumaa jioni, mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee alimtembelea hospitalini na kushiriki muda naye.

"Nilimmiss rafiki yangu,mara ya mwisho nilitumia wakati naye kwenye harusi yangu, alinipa wakati wake wote. Leo yuko chini. Nitakaa naye hapa usiku huu, nicheze densi tu na kumchekesha,” Akothee alisema kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Mwimbaji huyo aliambatanisha taarifa yake na video yake akimdensia mbunge huyo wa muhula wa kwanza huku wimbo wa Diamond Platnumz 'Moyo Wangu' ukicheza. Densi ilipoisha, Jalang'o aliamka kwa usaidizi wa mikongojo na mwimbaji huyo akamkumbatia vizuri.

Akothee pia alitumia fursa hiyo kufunguka kuhusu upendo wake mkubwa kwa mtangazaji huyo wa zamani wa redio na akamtakia afueni ya haraka.

“Upendo nilionao kwa Jalang’o, hakuna anayeweza kuuondoa . Wakati mwingine, sijui niwape nini watu ninaowapenda ili waweze kujua jinsi na wanamaanisha nini kwangu. Pona haraka osiepna , nakupenda,” alisema.

Kando na Akothee, watu wengine mashuhuri ambao wamemtembelea Jalang’o hospitalini ni pamoja na Mbunge Babu Owino,mjasiriamali Alinur Mohamed, mwimbaji Dufla Diligon,  Ian Oparanya, Rodgers Kipembe na MCA Abass Khalif.

Jalang’o alifanyiwa upasuaji Ijumaa baada ya kupata jeraha kwenye mguu wake wa kushoto alipokuwa akicheza mchezo wa mpira wa vikapu mnamo Septemba 27. Kisha alipelekwa katika Hospitali ya Nairobi ambako uchunguzi wa MRI ulifanyika.

Wakati akifichua habari kuhusu jeraha hilo kwenye video siku ya Jumatano, aliitaja kama "jeraha la kwanza la msimu."

Baada ya kupata jeraha hilo, kundi la watoa huduma ya kwanza walionekana wakishughulikia mguu wake uliojeruhiwa kabla ya kumshauri atembelee hospitali na kufanyiwa uchunguzi wa MRI mara moja.

“Nitaenda hospitali leo. Nimetengwa. Nitaenda kwa MRI," alisikika akisema. 

Baadaye alidokeza kuwa uchunguzi wa MRI ulibainisha jeraha lake lilihitaji matibabu maalum, jambo lililopelekea yeye kulazwa.

"Nilithani ni jeraha ndogo,.. natabasamu kwenye mashine ya MRI," alisema huku akionyesha akifanyiwa uchunguzi wa MRI.