Muigizaji Wema Sepetu hatimaye amevunja ukimya baada ya mama yake mzazi Bi Mariam Sepetu kumkemea hadharani kuhusu uhusiano wake na Whozu wakati wa sherehe ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa iliyofanyika Alhamisi jioni.
Bi Mariam alipopewa nafasi ya kutoa hotuba yake wakati wa karamu ya bintiye siku ya Alhamisi, aliyakashifu kwa hasira mahusiano yake na Whozu akibainisha kuwa hajabariki muungano huo.
Kufuatia kile ambacho huenda alihisi kuwa ni kudhalilishwa hadharani, Wema Sepetu sasa ameitaja usiku huo kuwa siku yake ya kuzaliwa mbaya zaidi kuwahi kutokea huku akibainisha kuwa hakufurahia kabisa, kinyume na nia yake ya awali.
“Nia na Madhumuni yangu ilikuwa ni kutaka kusherehekea siku yangu ya kuzaliwa na kuenjoy na wapenzi wangu ila haikuwa vile nilivyotarajia... Inshort shughuli yangu iliharibika sana... Lengo langu halikutimia,” Wema Sepetu alisema katika taarifa aliyoichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram. siku ya Ijumaa jioni.
Alikiri kuumia moyoni mwake na hata akadokeza kuwa huenda asifanye sherehe nyingine ya siku ya kuzaliwa baada ya kile kilichotokea.
“ Nimejitahidi kufanya kitu kizuri ambacho kingenifurahisha sana siku ya Birthday yangu ila haijakuwa. Najiskia vibaya sana. This was the worst Birthday Party of my Life na nahisi sitokuja fanya Party tena kwenye maisha yangu. Naumia moyoni mwangu ila kila kitu kinatokea kwa sababu... Ndo maana acha tu niseme "Alhamdulillah", alisema.
Miss Tanzania huyo wa zamani alidokeza kwamba alilazimika kutoa uchungu wake huo moyoni akisema “Ningekaa kimya ningekufa.” .
Siku ya Alhamisi usiku, Wema alibaki ameduwaa baada ya mama yake kumkemea kwa kujivunia mahusiano na mwanaume ambaye hajatambulishwa rasmi kwenye familia..
Bi Mariam Sepetu alifichua kuwa alihisi kutoheshimiwa na bintiye na mpenzi wake kwani walikuwa wameweka uhusiano wao hadharani bila hata kutafuta baraka zake. Aliendelea kuongeza kuwa ukiwa mtoto ni jambo la msingi kuwajulisha wazazi wako una uhusiano na nani na kumfahamu mtu ambaye una uhusiano naye.
"Nataka heshima itawale. Nataka wazazi waheshimiwe kama mtoto, lazima umsikilize mzazi wako. Kwa mpenzi ni lazima uje kujitambulisha," alisema Mariam kwa hasira.
Bi Mariam alifafanua kuwa hakuwa akijaribu kuelekeza maisha ya bintiye au kumzuia kupata mapenzi ila alichokuwa akiomba ni heshima tu, bila kulazimika kujua undani wa maisha ya bintiye mtandaoni. Aidha, alishikilia kuwa alikuwa akifanya haya yote kwa sababu ya upendo mkubwa alionao kwa binti yake.