Malkia wa Bongofleva Zuhura Othman almaarufu Zuchu ameweka wazi kuwa hakuna ugomvi wowote kati yake na mama mkwe wake Sanura Kassim almaarufu Mama Dangote.
Akizungumza katika mahojiano na Wasafi Media, msanii huyo mzaliwa wa Zanzibar alifichua kuwa uhusiano wake na mama mzazi wa Diamond Platnumz bado ni mzuri licha ya madai mengi ya ugomvi baina yao kwenye mitandao ya kijamii
Alifichua kwamba amekuwa na mawasiliano ya karibu na Mama Dangote na kudokeza kuwa hajaona mabadiliko yoyote katika uhusiano wao.
“Tuko vizuri. Niliongea naye kuhusu mipango ya kufanya birthday ya Simba. Kama familia lazima umshirikishe mama mtu.Tulishauriana na nini, yaani, tuko sawa.Hayo ni mambo tu ya mitandaoni lakini tuko sawa. Hakuna tatizo lolote ninalolijua,” Zuchu alisema.
Binti huyo wa Khadija Kopa alibainisha kuwa hatua ya Mama Dangote na Tanasha Donna kupeana zawadi, na mama huyo wa Diamond kudaiwa ku-munfollow kwenye Instagram hakukumaanisha tatizo lolote kati yao.
“Sisi wote kama Wasafi ni familia. Yule ni mama yetu na hakuna chochote kibaya. Ni mitandao tu inapenda mambo lakini tunaongea. Tuko vizuri,” alisema.
Huku akizungumzia uhusiano wake na bosi huyo wa WCB, Zuchu alikiri kwamba hana uhakika iwapo utapelekea ndoa kwani inaweza kuwa ni muungano wa muda.
Tetesi za mzozo kati ya Mama Dangote na Zuchu ziliibuka mwishoni mwa mwezi uliopita baada ya mama huyo wa Diamond kudaiwa kum-unfollow binti huyo wa Khadija Kopa kwenye mtandao wa Instagram. Mama Dangote pia alidaiwa kukubaliana na maoni ya shabiki aliyependekeza Diamond kurudiana na Tanasha na kumtimua Zuchu.
Wakati akijibu tuhuma hizo, Mama Dangote aliweka wazi kuwa hajamfuata wala kum-unfollow mtu yeyote kwenye Instagram katika siku za hivi majuzi.
“Mimi wasije wakaniingiza kwenye mambo yao. Mimi sijamu-unfollow. Niliowa-follow hao hamsini, ndio hao hao hamsini. Sasa nimuunfollow kwa kipi?” Mama Dangote aliiambia Wasafi Media.
Aliongeza, “Mimi mwenyewe ata nikigombana na mtu atajua mwenyewe. Niliowa-follow ni hao hamsini ,sina hamsini na moja. Mambo ya kitoto ya zamani wasiniingize. Mimi najijua mtu mzima. Mimi nimuunfollow amenifanya nini?”
Mamake Diamond aliwasihi wanamitandao kuepuka kumuingiza kwenye ugomvi na Zuchu huku akimtaja malkia wa Zanzibar kama bintiye.
“Wasinigombanishe na mwanangu Zuchu. Mimi sina ugomvi na mtu. Wasiniingize kwenye mambo hayo,” alisema.