Mwanamuziki na mratibu wa hafla, Weezdom amemtaja mwigizaji kutoka Tanzania, Wema Sepetu kuhusu tabia yake anayodai inamgharimu pesa, amani ya akili na afya ya akili.
Katika chapisho kwenye mtandao wa Insta stori, Weezdom alisimulia kuwa kitambo aliandaa ziara ya Wema Sepetu ya Kenya na pamoja na uongozi wake kwa klabu za hali ya juu jijini Nairobi na Mombasa.
"Wema Sepetu ni mmoja kati ya watu ambao walifanya nikazama kwenye msongo wa mawazo hapo awali ila nashukuru Mungu nilirudi kuwa sawa.Nilipanga safari yake ya ndege kuja Kenya yeye pamoja na uongozi wake ndani ya tarehe tofauti kwa Hoteli tofauti za kifahari za Nairobi na Mombasa."
Walitangulia kuweka nafasi za safari za ndege na malazi ili kuhakikisha kwamba kukaa kwake Kenya kunaenda sawa.
Siku ambayo Wema alitakiwa kufika Kenya, Weezdom anasema alipiga simu kwa wanablogu ili kuenda uwanja wa ndege kumlaki ila juhudi hizo zikagonga mwamba.
Mpango huo haukuenda vizuri kwani alifahamishwa kuwa mwigizaji huyo alikosa safari ya ndege kwa sababu ambazo hazingeweza kuhepukika.
"Mpaka nikaita wanablogu kwenye uwanja wa ndege waje tumsubiri,ila hakufika,alikosa safari ya ndege kwa sababu alilewa."
Weezdom alisema alilipa tikiti nyingine ya ndege na safari hii, jambo lile lile lilifanyika na hakuweza kusafiri hadi Nairobi.
Alishiriki kwamba alilazimika kurudisha malipo yote ya gharama hiyo, ambayo anasema ilikuwa hasara kubwa kwa upande wake.
Aliongeza kuwa amebakiwa na deni kubwa ambalo bado analilipa hadi sasa. Alimkashifu Wema kwa kuonyesha utu duni lakini yeye ni chapa kubwa.
Weezdom alidai tukio zima lilimfanya aanguke kwenye msongo wa mawazo na hajafanikiwa kumsamehe sosholaiti huyo.