Kwa wiki ya pili sasa ugomvi na kutupiana maneno baina ya muigizaji na mshawishi wa mitandaoni Wema Sepetu na mamake umekuwa ukigonga vichwa vya habari baada ya mama mtu kufumania hafla Wema aliyomwandalia mpenzi wake akidai kwamba haiwezekani mwanawe aishi na mtu kama mpenzi pasi na kumtambulisha nyumbani.
Wikendi mama huyo alifanyiwa mahojiano na Global TV Online ambapo alikariri kwamba bintiye Wema badi hajajitambua na wala hajielewi katika kile anachokifanya.
Mamake Wema alisema kwamba kinyume na DC wa Korogwe Jokate Mwegelo ambaye anajitambua na kuwa na mustakabali mwema, bintiye bado anasuasua sana.
Alizungumzia bintiye Wema kugombea ubunge Singida kwa wakati mmoja lakini akafeli na kusema kwamba alikata tamaa mapema na kujiharibia katika safari ya siasa ambayo alimfungulia mwenyewe.
“Wema yuko vizuri kwa kupata uongozi, lakini kama bado hajajitambua mwenyewe ni ngumu kwa mtu yeyote, hata kama mimi nisipojitambua ni ngumu. Kwa umri wangu, mimi napenda mtoto ajitambue, ajue yeye ni nani na afanye kazi zile zinazotakikana. Lakini swala ni kwamba nimejaribisha, kwa sababu kumpeleka Singida ni mimi kwa sababu kule ni kwetu,” alisema.
“Wema anatakiwa ajitambue, na akijitambua atafika mbali kwa sababu umri wake bado mdogo,” aliongeza akisema kwamba alitarajia Wema angekuwa mrithi wa kisiasa wa babake lakini hilo halijatokea.
Tamko la kuambiwa kwamba hajajitambua lilionekana kutomfurahisha Wema ambaye kupitia Instagram yake aliandika kwamba mamake amevuka mipaka sasa na pahali imefikia imetosha.
Wema alimwambia mamake kujishughulisha na ya kwake akisema kwamba kupangiwa maisha si jambo la kumfurahisha kwani yeye ameshakua na ana uwezo na uhuru wa kufanya maamuzi yake binafsi.
“Fanya kile kinachokupa wewe furaha... Ishi vile utakavyo wewe aslong as haileti madhara kwa mtu yoyote na uko na Positive Energy , ISHI... Life is too short to live kwa ajili ya kumfurahisha mtu mwingine & not yourself... Kila mtu afanye kile kinachomfurahisha yeye nafsi yake na sio kumridhisha mtu mwingine... Afu pia kupangiana maisha pia sio kitu kizuri...” alimjibu mamake.