logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Babake Diana Marua aridhika baada ya Bahati kutoa mahari, awabariki wafunge ndoa rasmi

Bahati alifichua kuwa babake Diana Marua, Mzee Omach aliwabariki na kuwapa mwanga wa kuoa rasmi baada ya mahari.

image
na Samuel Maina

Burudani18 October 2023 - 05:34

Muhtasari


  • •Bahati alifichua kuwa tayari amemtolea mahari mama huyo wa watoto wake watatu na akadokeza kuwa watafunga ndoa hivi karibuni.
  • •Bahati alibainisha kwamba alitaka sana kukamilisha malipo ya mahari ya Diana Marua kabla ya kuadhimisha miaka 7 ya uhusiano wao.

Ni wazi kuwa wanandoa mashuhuri wa Kenya Kelvin ‘Bahati’ Kioko na Diana Marua wanakaribia kuifanya ndoa yao kuwa rasmi.

Siku ya Jumanne, Bahati alifichua kuwa tayari amemtolea mahari mama huyo wa watoto wake watatu na akadokeza kuwa watafunga ndoa hivi karibuni.

Katika taarifa yake, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 30 alifichua kuwa babake Diana Marua, Mzee Omach aliwabariki na kuwapa mwanga wa kuoa rasmi baada ya mahari.

“Ni rasmi!! Hatimaye nimefanya malipo ya mahari ya Diana Marua na baba yetu mzee Omach ametubariki kuendelea na mipango ya harusi,” Bahati alisema kupitia Instagram Jumanne.

Mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili aliambatanisha taarifa hiyo na video ya babake Diana Marua akiwabariki na kuwaombea. Katika video hiyo, wenzi hao walishikana mikono huku Mzee Omach akiwaombea. Wote wawili walikuwa wamevalia vitenge vya njano.

“Mungu warehemu Diana na Kelvin. Kwa yote wanayowaza, yote wanayotamani, yote wanayonena na vinywa vyao pamoja na yote wanayotenda, yawe ya kukusifu na kukukutukuza wakati wote,” Mzee Omach aliomba.

Bahati alibainisha kwamba alitaka sana kukamilisha malipo ya mahari ya Diana Marua kabla ya kuadhimisha miaka 7 ya uhusiano wao mnamo Oktoba 20.

Kwa upande wake, Diana Marua alisema kuwa malipo ya mahari ni zawadi bora zaidi ambayo mumewe amempa na kumhakikishia kumpenda sana.

"Zawadi yangu bora bado. Kwa yule ambaye mbingu ilinitayarishia, ninaahidi kufanya kile ambacho Biblia inaniamuru kufanya. Kukupenda na kukuheshimu siku zote za maisha yangu. Siwezi kusubiri kusema Ndiyo ninafanya. Asante Babe,” Diana Marua alimwambia mumewe.

Bahati alimchumbia rasmi mzazi mwenzake Diana Marua mwezi Juni baada ya kuwa kwenye mahusiano kwa muda mrefu.Walirekodi kipindi hicho katika video iliyopeperushwa kwenye chaneli ya YouTube ya Diana Marua.

Wakati akichukua hatua hiyo kubwa, Bahati alibainisha kuwa amekamilisha hatua zote muhimu kuelekea ndoa na sasa yuko tayari kuifanya rasmi.

"Umenipatia moyo wako. Kusema kweli kutoka ndani ya moyo wangu, siichukulii virahisi. Kitu kimoja ambacho ninataka sana kufanya mwaka huu, nataka tu kuhakikisha nimefanya sawa, najua nimeenda kwa familia yako kwa utambulisho lakini mwaka huu nataka tufanye harusi ya kweli na nataka kukuoa," Bahati alimwambia mchumba wake.

Aliongeza, "Nataka kuhakikisha kwamba nimekuoa kiroho rasmi. Mungu anajua moyo. Nataka kuifanya kwa utamaduni. Kwa heshima ya wazazi wako, baba yako, nakuahidi kwamba mwaka huu nitakufanyia harusi kubwa na bora zaidi ambayo macho yako yamewahi kuona. Hiyo ndiyo ahadi yangu."

Pindi tu baada ya kusema maneno hayo matamu kwa Diana ambaye wakati huo tayari alikuwa amezidiwa na hisia kali, mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili alitoa pete ambayo alikuwa ameibeba kwenye kasha dogo na kisha kumuuliza mama huyo wa watoto wake watatu iwapo ataolewa naye.

"Nataka kuchukua fursa hii kukuonyesha kwamba namaanisha hilo na nakuthamini. Ndiyo maana nataka kufanya upya viapo vyetu. Nataka kukuuliza kwa mara nyingine, "Je, utaolewa nami?" alimuuliza.

Huku akibubujikwa na machozi, Diana Marua alijibu, "Ndiyo. Nakupenda sana na nasema ndiyo mara milioni. Na asante."


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved