Staa wa Bongofleva, Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz ameendelea kuonyesha wazi kwanini yeye ni ‘Simba’ na kwanini anafaa kutambuliwa kama mmoja wa wasanii matajiri na wanaoheshimika barani Afrika.
Siku ya Ijumaa, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 32 alionyesha kwa majivuno ndege yake ya bei kifahari, ambayo ni moja tu ya vitu vya gharama kubwa ambavyo anamiliki.
Diamond alionyesha ndani na nje ya ndege hiyo ya kibinafsi wakati yeye na familia yake walikuwa wakipanda kwenda katika nchi jirani ya Rwanda kwa ajili ya Tuzo na Tamasha la Trace.
“Kigali, Rwanda one time for the @traceawardsandfestival,” Diamond aliandika chini ya video hiyo ambayo alichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Katika video hiyo, msanii huyo na watoto wake watatu; Tiffah Dangote, Prince Nillan na Naseeb Junior walionekana wakikaribishwa ndani na rubani mzungu na mhudumu wa ndege.
Kisha bosi huyo wa WCB alionekana akiwaonyesha watoto wake ndani ya ndege hiyo ya kifahari ambapo kila kitu kiliandikwa ‘Diamond Platnumz’.
"Kila kitu ni cha Platnumz, unataka kuona nini? NJ unataka kuona nini?" Diamond alisikika akiwaambia watoto wake.
Watoto hao watatu walionekana kushangazwa na kuvutiwa na mafanikio ya baba yao walipokuwa wakitembea ndani ya ndege ya kibinafsi.
Watoto wa Zari, Tiffah na Prince Nillan ambao walionekana kufurahishwa zaidi walisikika wakimuuliza baba yao kwa mshangao mkubwa iwapo wanaruhusiwa kutumia chombo hicho cha usafiri wakati wowote wanapotaka.
“Ni Diamond Platnumz, Oh my God, Napenda ndege hii.. tunaweza kutumia wakati wowote? Wakati wowote, popote?" Tiffah na Nillan walisikika wakisema.
Diamond aliwahakikishia watoto wake kwamba wanaruhusiwa kusafiri kwa ndege ya kibinafsi wakati wowote wanapojisikia wanataka.
Staa huyo wa Bongofleva alitangaza mpango wa kununua ndege ya kibinafsi mapema mwaka uliopita.Alifichua kuhusu mpango wake wakati akimtakia meneja wake El-Jefe Mendez heri za siku ya kuzaliwa.
"Tulinunua 2021 Rolls Royce Black Bedge Zero Kilometre mwaka jana, na tunanunua ndege ya kibinafsi mwaka huu!! hiyo ndio tafsiri ya kuwa na usimamizi bora!! Ni Siku ya Kuzaliwa ya meneja wangu Sallam Sk," Diamond aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.