Muigizaji maarufu wa Kenya Jackie Matubia amejibu maswali kuhusu kutokuwepo kwake wakati wa harusi ya kitamaduni wa marafiki zake Milly Chebby na Terence Creative.
Matubia ambaye hakuonekana popote wakati wa hafla hiyo ya kitamaduni iliyofanyika katika Kaunti ya Nandi siku ya Jumamosi alidokeza baadhi ya sababu zilizomfanya kutojitokeza kwa hafla hiyo baada ya mashabiki kumhoji kwenye Instagram.
Shabiki mmoja mwenye wasiwasi alitoa maoni yake kuhusiana na hafla hiyo akisema, ""Ata mkikosa kusema Jackie Matubia na Milly hawako in good terms juu hangekosa kitu kaa hii alafu offlate tumeona hawajakua karibu, nini hasa kilitokea."
Shabiki mwingine alionekana kukubali na kumtaja muigizaji huyo ili ajieleze, "Unajitetea ukiwa kipande gani?"
Huku akijibu kuhusu suala lililojadiliwa, mama huyo wa watoto wawili alidokeza kwamba aliambiwa hana fadhili na hana ndoa.
"Najitetea nini na washasema niko na roho mbaya na pia sina bwana," Matubia alijibu.
Mtumizi mwingine wa Instagram alimuuliza muigizaji huyo wa zamani wa kipindi cha Tahidi High, "Hukuhudhuria ruracio ya mpenzi wako?"
Matubia alimjibu shabiki huyo akisema, “Si unaniona hapa, mbona unauliza swali tayari na jibu?”
Kwa muda mrefu, Jackie Matubia na Milly Chebby wamekuwa marafiki wa karibu na walikuwa na uhusiano wa karibu sana hivyo mpenzi huyo wa zamani wa mwigizaji Blessing Lung’aho kukosa tukio la Jumamosi liwashangaza wengi. Mashabiki waliachwa wakijiuliza nini kilitokea kwa marafiki hao wawili ambao mara nyingi walionekana wakisherehekea matukio muhimu na hafla maalum pamoja..
Urafiki wa wanawake hao wawili ulionekana kuanza kufifia miezi michache iliyopita baada ya kutoonekana wakiwa pamoja kama zamani.
Tofauti na hapo awali, Milly Chebby alikosa kuchapisha chochote kuadhimisha sherehe ya binti wa kwanza wa Jackie Matubia mnamo Julai. Hili liliwaacha mashabiki wakikisia kuwa kuna kitu kibaya.