Mzalishaji mwanzilishi wa midundo ya Gengetone Magix Enga amejitokeza kwa mara ya kwanza na kulia kwa uchungu jinsi ambavyo amekuwa akitaabika kutokana na mitikasi yake yote kubuma.
Enga kupitia ukurasa wake wa Facebook, alipakia picha yake akiwa amempakata mwanawe wa mwezi mmoja na kulia kwamba amejitahidi sana kuficha machungu yake lakini amefika mwisho kwani kila kitu ambacho anajaribu kukifanya kwa sasa hakileti tija.
Enga amefunguka kwamba licha ya kufanya kazi nyingi zilizotamba na wasanii wengi, hajawahi faidika kifhedha kutoka kwa kazi hizo hata moja, akitaja baadhi ya ngoma alizozizalishia midundo na kufanya vizuri lakini hajawahi faidika.
“Magix Enga, mfalme mwenye talanta wa beat barani Afrika kote na duniani. Baadhi ya wasanii niliofanya nao collabo walinufaika na Mimi. Nyimbo nyingi nilizotayarisha I.e (dundaing ,watoto na pombe Otile brown ft Enga and mejja , mapenzi hisia) na nyingine nyingi ambazo sinufaiki nao,” alisema.
Msanii huyo alisema kwamba licha ya mambo kumuendea mrama, bado anaamini kwamba yeye bado ndiye mzalishaji bora wa beat na kuendelea kuthibitisha hilo kwa kutaja baadhi ya kazi zenye midundo ya kuvutia alizowahi kuzalisha.
“Bado naamini mimi ndiye mtayarishaji bora. Mfano wimbo wa Gengetone watu waliupenda yaani wimbo unaokanyaga zaidi ni Mamiondoko ambao sijafaidika nao, Digidigi kutoka kwa Arrow boy ambao una views zaidi ya 10,000,000 sijapata hata senti moja kutoka kwake. Kwa sasa sina kazi,” alilia.
Alimalizia kusema kwamba yeye ni baba mpya mwenye mtoto wa kiume mwenye umri wa mwezi mmoja ambaye anamtegemea lakini hana namna ya kumpa malezi bora.
Enga alimuomba rais Ruto kumpa msaada kuanzia kifedha hadi kwenye mkwamuo wa kisanaa.
“Sasa hivi naandika haya nina mtoto wa kiume wa mwezi 1 ambaye ananitegemea. Nilijaribu kujivuta lakini studio niliyokuwa nafanyia kazi ilifungwa kwa sababu ya masuala ya kukodisha. Rais wetu DR.William Samoei Ruto naweza kukuomba unisaidie katika usaidizi wowote unaoweza kuanzia tasnia ya muziki,” alimaliza.