Seneta Karen Nyamu ajibu shinikizo la mpenzi wake Samidoh kutumwa Haiti

Nyamu alipendekeza kuwa nchi hiyo iliyojaa machafuko inapaswa kuhamishwa hadi Kenya badala yake.

Muhtasari

•Mwanamtandao alipendekeza Samidoh anafaa kutolewa kwa nchi hiyo ya Amerika Kaskazini pamoja na maafisa wengine watakaotumwa huko.

•Nyamu alisema ana imani kubwa kuwa Kenya itapata mafanikio makubwa kwa kuongoza oparesheni ya usalama  nchini Haiti.

amejibu shinikizo la Samidoh kutumwa Haiti
KarenNyamu amejibu shinikizo la Samidoh kutumwa Haiti
Image: HISANI

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu alitoa jibu la kejeli baada ya mtumiaji wa mtandao wa Facebook kupendekeza mpenzi wake, Samuel Muchoki almaarufu Samidoh kuwa miongoni mwa maafisa wa polisi watakaotumwa nchini Haiti kwenye misheni ya kulinda amani.

Chini ya moja ya machapisho ya Facebook ya mwanasiasa huyo mwenye utata, mwanamtandao mmoja alipendekeza kwake kwamba mwimbaji huyo wa Mugithi anafaa kutolewa kwa nchi hiyo ya Amerika Kaskazini pamoja na maafisa wengine watakaotumwa huko.

"Sasa Samidoh atumwe Haiti," mwanamtandao Boybey Joe aliandika chini ya chapisho la seneta Nyamu.

Katika jibu lake, seneta huyo wa kuteuliwa wa UDA alipendekeza kuwa nchi hiyo iliyojaa machafuko inapaswa kuhamishwa hadi Kenya badala yake.

“Labda Haiti ije huku,” Karen Nyamu alijibu.

Mapema mwezi huu, Nyamu alisema ana imani kubwa kuwa Kenya itapata mafanikio makubwa kwa kuongoza oparesheni ya usalama  nchini Haiti.

Kama Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya Usalama wa Kitaifa, Ulinzi na Uhusiano wa Kigeni, Nyamu alisema kuwa nia ya Kenya kuchukua operesheni hiyo, kwanza ni kudhihirisha ulimwengu kuwa Kenya ni nchi ya kutegemewa.

"Kenya ina historia ya kulinda amani na tumehusika katika nchi kama vile Somalia. Huu ni ujumbe wa usalama unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na nchi nyingine mbali na Kenya ambazo  zinahusika ," alisema.

Katika mazungumzo na runinga ya K24, seneta Karen Nyamu aliongeza kuwa Kenya inasimama kama nchi ya kutegemewa.

"Na kuna nini kwetu? Kenya inajitokeza kama mshirika wa kutegemewa ambayo ni faida kubwa sana kwetu kaama Taifa. Tunatoa kauli kubwa sana kwamba Kenya ni taifa linalotegemewa," alisema.

Aliongeza kuwa kando na  kutumwa Haiti, polisi wa Kenya watafaidi na kozi za mafunzo ya hali ya juu zinazowezeshwa na wafadhili wa misheni.

"Kabla ya polisi hawa kwenda Haiti, watapata mafunzo. Tuseme ukweli tunaweza kuwa hatuna vifaa kwa sasa na ndio maana hatuna tarehe ya kupelekwa lakini mafunzo yatakuwa mazuri kwa vikosi vyetu," Seneta alisema.

Aidha, seneta Nyamu alibainisha kwamba Kenya pia itapata fedha kutokana na kuongoza operesheni ya kulinda amani Haiti.

"Motisha za kifedha pia zinahusika. Tunapozungumza hivi sasa Marekani na nchi nyingine zinazotaka kusaidia misheni zimetoa dola milioni 200 kwa misheni hii," alisema.

Mwanasiasa huyo mwenye utata mwingi aliongeza kwa kueleza majukumu ya kikosi ambacho kitatumwa kwenye operesheni hiyo akisema Kikosi cha Kenya, kinakusudiwa kuimarisha sheria na utulivu wa sehemu hizo.