Mama mzazi wa mtayarishaji maudhui mashuhuri Purity Vishenwa almaarufu Pritty Vishy amejitokeza na kufichua kuwa hayuko sawa kisaikolojia.
Katika video iliyochapishwa kwenye chaneli ya YouTube ya Pritty Vishy, mama huyo ambaye amekuwa akifanya kazi nchini Saudi Arabia kwa miaka mitano iliyopita alifunguka kuhusu jinsi alivyokumbwa na msongo wa mawazo katika kipindi cha siku chache zilizopita baada ya mahojiano ambayo alifanya kusambaa.
Aidha, alisikitika kuwa watu walikosa kuelewa matamshi yake kuhusu ‘Ben 10’ ambayo alitoa wakati wa mahojiano yake na Mungai Eve hivi majuzi.
“Mimi niko na stress kwa sababu kulingana na vile watu wa mitandao ya kijamii wamebeba stori, najiuliza nitapeleka wapi masikio. Mimi ni mtu niko na familia, niko na marafiki,” mama ya Pritty Vishy alilalamika kwenye video hiyo iliyowekwa Ijumaa.
Mamake Vishy alilalamika kwamba watu waliyaelewa visivyo matamshi yake kuhusu ‘Ben 10s’ na kubainisha kuwa hakuna wakati alimaanisha kwamba anatafuta mmoja.
“Mimi nilisema, sihitaji Ben 10. Lakini pia nikatumia lugha ya kusema, Ben 10 wote ambao wanasikiliza hiyo video wasione kama kwamba nasema hawajakomaa. Nilisema kuna wale wamekomaa,” alisema.
Mamake Vishy zaidi alizungumzia masaibu ya mwanamke ambaye yupo kwenye mahusiano na mwanamume mdogo kiumri akisema kwamba ni wachache sana kati yao wanaochukulia uhusiano huo kwa uzito.
“Wengi wao huwa wanadate wakijua wanadate kama sugar mummy. Mwingine anasema nachukua muda hapa tu nikule chenye nataka. Nilisema sitaki kuweka watu wote katika kitengo hicho. Nilisema kuna wale mature. Lakini sikumaanisha nataka,” alisema.
Mama huyo wa mpenzi huyo wa zamani wa Stevo Simple Boy alifichua kuwa aliumia sana baada ya kuona maneno makali na matusi ambayo alitupiwa baada ya mahojiano hayo kupakiwa.
Alitoa wito kwa watu kutomnukuu vibaya akisema kwamba inaweza kusababisha shida kwa mahusiano ya binti yake kwani amefikia umri wa kuolewa.
“Mimi nimekaa Saudi Kemboi kwa miaka miaka. Sijawahi kuwa ndani ya mahusiano. Wengi wanatazama watakwambia Kemboi’s ako na uhuru kiasi gani. Mimi nimetoka Saudia bila kupatana na mwanaume yeyote. Nilikuwa na dereva wangu wa base. Alikuwa anakuja ananitoa kwa nyumba ananipeleka kazi na mahali popote nataka. Nilikuwa nampa heshima yake na sikuonyesha ati niko desperate. Kwa miaka nimeishi Saudia bila mtu, bila kutumiwa. Nitakuwa hapa nimeingia kutafuta Ben 10,” alisema Mamake Pritty Vishy.
Pritty Vishy pia alithibitisha kuwa mama yake amekuwa hafanyi vizuri kisaikolojia baada ya mahojiano kutolewa.