Usiku wa Jumatatu wapenzi wa soka duniani walishuhudia tukio kubwa la soka ambapo ‘mchawi’ wa soka kutoka Argentina, Lionel Messi alijishindia tuzo ya Ballon d’Or kwa rekodi ya mara nane, Zaidi ya mchezaji yeyote yule kuwahi kutokea tangu kuasisiwa kwa tuzo hiyo ya kibinafsi kwa wanasoka.
Miongoni mwa mamilioni ya watu kutoka pembe zote duniani waliokuwa wanafuatilia kutolewa kwa tuzo hizo ni msanii Diamond Platnumz ambaye aliganda mbele ya runinga yake.
Ilipofika zamu ya mshindi kutajwa, Messi alijongea jukwaani na kukabidhiwa tuzo hiyo kabla ya wavulana wake 3 kujiunga na baba yao katika jukwaa.
Wakati huo huo kamera zilielekezwa kwenye hadhira ambapo mmoja wa walioudhuria katika ukumbi huo alikuwa mke wa Messi, Antonela Roccuzzo.
Wakati Messi anapoonesha tuzo yake kwa mashabiki akiwa na vijana wake, Antonela hakuweza kuificha furaha yake na muda wote akijawa na tabasamu alizidisha kuwapiga makofi yasiyo na mwisho.
Tukio hili lilimgusa sana Diamond ambaye kando na kufuatilia pia alikuwa anarekodi kwa simu yake akizungumza.
Diamond alisema kwamba Antonela ni mfano bora sana kwa mwanamke bomba ambaye anasimama na mumewe katika hali zote, pia kumshangilia katika ushindi wake.
Aliwataka kina dada kuiga mfano huo na kukoma kutebwereka wakisubiria mwanamume mwenye mali na kila kitu kuwafuata wakati wanawatoroka wapenzi wao wasio na kitu pasi na kujua kwamba kesho yao huenda ikawa tofauti na yenye nafuu.
“Wanawake mnaona vile mtu hutoka mbali na mwenzake? Wakati anahustle. Lakini sasa nyinyi mnataka mwanaume ambaye ahsakuwa na hela badala ukwame na wako umpe moyo hadi afike mbali kama hivi, mnaona mwenenu anavyo enjoy?” Diamond alisema kwenye video hiyo aliyopakia kwenye Instagram story yake.