Wasanii Whozu, Billnass na Mbosso wamepigwa marufuku ya kujihushisha kwa njia yoyote ya Sanaa ya muziki Tanzania kufuatia kile kilichotajwa kuwa maudhui chafu kwenye remix ya wimbo wa ‘Ameyatimba’.
Baraza la Sanaa Tanzania, BASATA katika taarifa lilimtaka msanii Whozu, ambaye ndiye mwenye wimbo huo ambaye aliwashirikisha Mbosso na Billnass kwenye remix, kufuta wimbo huo mara moja kutoka kwenye majukwaa yote ya kidijitali ya kusambaza muziki.
Watatu hao walitimba studioni mapema wiki jana na kufanya remix ya Ameyatimba na kuachia video yake ambayo sasa imetajwa kuwa chafu na BASATA.
Kando na marufuku ya kutojihusisha na muziki kwa miezi mitatu, watatu hao pia kila mmoja alitakiwa kulipa fiani ya shilingi milioni 3 za kitanzania.
“Mnamo tarehe 2 Novemba 2023, mwanamuziki anayetambulika kwa jina la kisanii Whozu alichapisha video ya wimbo ‘Ameyatimba’ akiwashirikisha wasanii Mbosso na Billnass, wenye mauidhui yanayokiuka kanuni za maadili kutokana na kuwepo ishara ya vitendo vinavyoashiria kinyume na kanuni 25(6)(j) pamoja na vitendo vya unyanyasaji, ukatili na udhalilishaji wa utu wa mwanamke kinyume na kanuni…” sehemu ya taarifa ya BASATA ilisoma.
“Baraza limefuata uamuziufuatao; limemtaka mara moja kushusha video ya wimbo huo kwenye digital platforms zote, limemtoza faini ya shilingi milioni 3, na limemfungia kujishughulisha na Sanaa kwa muda wa miezi 6 kuanzia Novemba 4,” iliongeza taarifa hiyo.
Kwa wasanii Mbosso na Billnass walioshirikishwa, BASATA waliamuru;
“Aidha wasanii Mbosso na Billnass wametozwa faini ya shilingi milioni 3 kila mmoja na kufungiwa kutojishughulisha na kazi za Sanaa kwa muda wa miezi 3 kuanzia Novemba 4.”
BASATA walisema kwamba hii si mara ya kwanza kwa Whozu kupatikana na makosa ya maudhui yanayokwenda kinyume na kanuni za kimaadili ambazo zimeorodheshwa kwenye katiba ya baraza hilo.
“Msanii huyo ameshaonywa mara mbili na kutozwa faini mara moja huko nyuma kwa kukiuka taratibu za kuzingatia maadili katika kazi za Sanaa lakini bado anaendelea kupuuza,” walibaini.