Mzee Abdul Juma Isack, anayesadikiwa kuwa baba mzazi wa Diamond Platnumz amemuonya bosi huyo wa WCB dhidi ya kumtenga mtoto wa mwanamitindo Hamisa Mobetto.
Katika mahojiano na Mbengo TV, mzee huyo alimuagiza Diamond amthamini mwanawe Dylan Abdul Naseeb kama watoto wake wengine watatu. Mvulana huyo mwenye umri wa miaka 6 anaaminika kuwa mtoto wa mwimbaji huyo wa bongo na Hamisa Mobetto, hata hivyo kuna utata mwingi unaozunguka suala hilo.
Licha ya utata uliopo, Mzee Abdul amemtaka mwanawe kutowagawanisha watoto wake na badala yake awapende wote sawa.
“Mimi nataka athamini watoto. Kwa sababu ana mali nyingi sana kupita kiwango. Athamini watoto, atunze mali zake wakati alipo, asigawe watoto. Asifanye watoto wao katika masuala ya kuchukia baadaye,” Mzee Abdul alisema kwenye mahojiano hayo.
Alidokeza kuwa kwa kuwagawanya watoto wake, Diamond anaweza kuwaletea matatizo mengi katika siku za usoni wakati wa kugawana mali yake ukifika.
Zaidi ya hayo, Mzee Abdul alibainisha kuwa mwanawe ana mali ya kutosha hata kugawia hadi watoto kumi, hivyo hakuna haja ya yeye kumbagua mtoto wake yeyote.
"Asibague. Kitanda hakizai haramu. Hakizai haramu asibague mtoto. Mtoto hachaguliwi, hajui nani atakayekusaidia baadaye. Unayemuona mbaya baadaye ndiye atakubeba. Hamna chanzo kisichokuwa na mwisho,” alisema.
Mzee Abdul alidokeza kuwa Dylan ni mtoto wa Diamond na kumtaka asiruhusu masuala yake na mpenzi wake wa zamani Hamisa Mobetto kumfanya abague mvulana huyo.
"Naamini kama sio mtoto wake, basi angemkataa mahakamani," alisema.
Kwa kuongezea, babake Diamond alisema ikiwa matokeo ya DNA yalithibitisha kuwa mvulana huyo wa miaka sita sio mtoto wake, basi anaweza kuwa baba mlezi kwake.
“Kwa sababu alitoa ahadi yake ya kumtunza, basi afanye hivyo asimkane. Awe baba mlezi, kwani kwa mfano angemkuta (Hamisa) ana mtoto alafu akampenda jinsi alivyo, angemkataa mtoto? Afanye basi kama baba mlezi, hata kama DNA imetoka sio,” alisema.
Mzee Abdul alisema kuwa Dylan anaweza kuja kumsaidia staa huyo wa bongo fleva iwapo atakubali kuhusika katika maisha yake.