KBC yafichua sababu ya kutopeperusha mechi ya Harambee Stars baada ya kulaumiwa na waziri Namwamba

Mashabiki wengi wa soka waKenya walilamikia serikali na kituo hicho kwa kushindwa kupeperusha mechi ya Harambee Stars na Gabon..

Muhtasari

•Wasimamizi wa KBC wamewaomba radhi Wakenya na kueleza kuwa walishindwa kupeperusha mechi hiyo kufuatia changamoto ya kiufundi ya satelaiti.

• “Tuna deni la Wakenya la ombi la msamaha wa dhati, usio na shaka na usio na utata kwa kukatishwa tamaa huku," Waziri Namwamba alisema.

wakifanya mazoezi kabla ya mchuano dhidi ya Gabon.
Wachezaji wa Harambee Stars wakifanya mazoezi kabla ya mchuano dhidi ya Gabon.
Image: TWITTER// HARAMBEE STARS

Shirika la utangazaji la kitaifa la Kenya, KBC limetoa taarifa kuwaomba radhi wananchi kwa kushindwa kutangaza moja kwa moja mechi kati ya Harambee Stars na timu ya taifa ya Gabon siku ya Alhamisi usiku.

Mashabiki wengi wa kandanda wa Kenya walikuwa tayari wamewasha runinga zao mwendo wa saa moja usiku wa Alhamisi wakisubiri kufurahia mechi hiyo ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la FIFA ambayo ilichezewa jijini Franceville, Gabon lakini walikata tamaa kwani haikuonyeshwa kamwe.

Katika taarifa ya Ijumaa asubuhi, wasimamizi wa KBC waliwaomba radhi Wakenya na kueleza kuwa walishindwa kupeperusha mechi hiyo kufuatia changamoto ya kiufundi ya satelaiti.

"Tunaomba radhi kwa Wakenya kwa kushindwa kupeperusha mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la FIFA la 2026 kati ya Gabon na Kenya mnamo Novemba 16, 2023 saa moja usiku kutokana na changamoto ya kiufundi ya satelaiti," wasimamizi wa KBC walisema katika taarifa.

Shirika hilo la utangazaji la serikali ya Kenya hata hivyo limewahakikishia wakenya kuwa wataweza kutazama mechi zijazo za Harambee Stars kwani tatizo hilo limerekebishwa.

"Tafadhali kumbuka kuwa hii imerekebishwa na tunatazamia matangazo bila kukatizwa katika siku zijazo," taarifa hiyo ilisoma.

KBC ilitoa msamaha huo punde tu baada ya waziri wa Michezo na Sanaa Ababu Namwamba kulaumu runinga hiyo inayomilikiwa na serikali kwa kukosa kupeperusha mechi hiyo.

Waziri huyo katika taarifa yake alieleza kiini cha tatizo lililofanya mechi hiyo kutorushwa na kuwaomba radhi mashabiki wa soka wa Kenya kwa niaba ya kituo hicho.

"Jana usiku @KBCChannel1 iliwaangusha mashabiki wa Kenya kwa matatizo ya satelaiti ambayo yalisababisha kushindwa kuonyesha mechi ya Harambee Stars dhidi ya Gabon jijini Franceville," waziri Ababu Namwamba alisema katika taarifa yake Ijumaa asubuhi.

 Aliongeza, “Tuna deni la Wakenya la ombi la msamaha wa dhati, usio na shaka na usio na utata kwa kukatishwa tamaa huku. Hakika mnastahili bora zaidi. POLENI SANA.”

Kwa bahati mbaya, timu ya taifa ya Kenya haikufanikiwa kupata pointi hata moja nchini Gabon kwani ilichapwa mabao 2-1 na mwenyeji.

Masoud Juma aliiweka mbele Harambee Stars katika kipindi cha kwanza baada ya kufunga bao katika dakika ya 40. Hata hivyo, mabao mawili, ya Denis Bouanga na ya Guelor Kanga katika kipindi cha pili yaliwapa wenyeji ushindi mwishoni mwa mechi hiyo ngumu.